Mtibwa Sugar yaweka mikakati mechi ijayo

Bingwa - - HABARI - NA ZAINAB IDDY

BAADA ya kufanikiwa kuingia raundi ya pili ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Uongozi wa Mtibwa Sugar umesema kuwa hakuna kulala kwani tayari wameshaweka mikakati kwa ajili ya mechi yao inayofuata.

Mtibwa Sugar imesonga mbele katika mashindano hayo, baada ya juzi kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Northern Dynamo katika mchezo wa marudio uliochezwa kwenye visiwa vya Shelisheli juzi.

Kabla ya mechi hiyo, Mtibwa Sugar ilipata ushindi wa 4-1 wakiwa nyumbani, hivyo kuwafanya wasonge mbele kwa jumla ya mabao 5-1.

Matokeo hayo yanawapa nafasi Mtibwa Sugar kukutana na KCCA ya Uganda, mchezo utakaochezwa Desemba 14 mjini Kampala kabla ya timu hizo kurudiana wiki moja baadaye jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wakatamiwa hao, Swaburi Abubakar, ameliambia BINGWA jana kuwa timu yao ilitarajia kurejea nchini jana na kwenda moja kwa moja mjini Morogoro watakapoweka kambi.

“Tumu inawasili leo (jana) na kwenda moja kwa moja mkoani Morogoro mjini, tutakapoweka kambi kujiandaa na mechi yetu inayokuja kwani hatuna muda wa kupoteza hivi sasa.

“Tunahitaji kufika angalau hatua ya nusu fainali, hivyo lazima tujipange katika mashindano haya hakuna timu ya kuidharau katika hili, lazima wachezaji wajitume na sisi viongozi tukamilishe mahitaji yao kwa wakati sahihi ili kutowavunja nguvu,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.