HAWAKUW NA Hapa ndipo Modric alipowabwaga Messi, Ronaldo CHAO Ballon d'Or

Bingwa - - EXTRA - MADRID, Hispania

HATIMAYE usiku wa kuamkia juzi historia iliandikwa baada ya nyota wa Real Madrid, Luka Modric, kutangazwa kuwa mchezaji bora mpya wa mwaka wa dunia na kukabidhiwa tuzo ya Ballon d'Or, akiwabwaga vinara, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, waliotamba nayo kwa muda wa miaka 10.

Tuzo hiyo ni moja kati ya mafanikio aliyoyapata kwa mwaka ikiwa ni baada ya nyota huyo wa timu ya Taifa ya Croatia hivi karibuni kunyakua tuzo za mchezaji bora wa mwaka wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) la kimataifa Fifa.

Hata hivyo, tuzo hii ya Ballon d'Or ndiyo inayoonekana kilikuwa ni kibarua kikubwa kwake kutokana na kuwa alikuwa akishindana na mastaa waliowahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia wakiwamo, Antoine Griezmann, Kylian Mbappe na Raphael Varane, bila kutaja mchuano mwingine kutoka kwa wababe, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Licha ya kukabiliwa na ushindani huo, Modric, aliweza kukomaa hadi mwisho akitumia kiwango chake na mafanikio aliyoyapata ndani ya mwaka huu na huku akisaidiwa na vigezo vingine hadi kufikia anatangazwa kuwa mchezaji bora wa sayari hii kwa mwaka huu.

Katika makala haya wachambuzi wa masuala ya soka wamejaribu kuchambua mambo manne ambayo yalimfanya staa huyo aibuke mshindi wa tuzo hiyo ya Ballon d'Or.

1.Watu walitaka mabadiliko

Licha ya Modric kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo ya Ballon d'Or kwa mwaka huu, lakini bado kuna mjadala unaoendelea kama ni kweli alistahili kuwafunika Lionel Messi na Cristiano Ronaldo na mjadala huo utaendelea kuwapo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, staa huyo raia wa Croatia, amekuwa na kiwango kizuri katika mashindano yote mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na fainali za Kombe la Dunia na mafanikio mengine ambayo ameyapata kwa mwaka huu yanayomfanya astahili kunyakua tuzo hiyo ya Ballon d'Or.

Msimu uliopita, Messi aliumaliza akiwa mfungaji bora wa La Liga na ligi kubwa tano Ulaya na vile vile aliisaidia Barcelona kutwaa mataji mawili ya ligi ya ndani na huku Ronaldo akiwa kinara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiiongoza Real Madrid kutwaa kwa mara ya tatu mfululizo ubingwa wa michuano hiyo na pia akimaliza akiwa mfungaji bora kwa mara ya sita mfululizo bila kuhesabu mabao 40 aliyoifungia klabu hiyo katika kipindi hicho.

Hata hivyo, bila kuongopa pamoja na mastaa hao kufanya hivyo, Modric alistahili tuzo hiyo ya Ballon d'Or kwa kiwango na mafanikioa aliyoyapata ndani ya mwaka huu.

Lakini kama utakuwa na kumbukumbu kilichowahi kuwatokea mastaa kama Xavi na Iniesta mwaka 2010, Frank Ribery, mwaka 2013 na mlinda mlango, Manuel Neuer, mwaka 2014, unaweza

kubaini kwamba watu walihitaji mkono mwingine mpya wa kunyanyua tuzo ya Ballon d'Or na ndio maana wakampigia kura Modric.

2. Messi na Ronaldo walichemka nchini Urusi Sababu nyingine ambayo ilimsaidia Modric kuondoka na Ballon d'Or kwa mwaka huu ukweli ni kwamba nyota wa Barcelona, Lionel Messi na mwenzake wa Juventus, Cristiano Ronaldo, walishindwa kung’ara wakiwa na timu zao za taifa katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka huu nchini Urusi. Kabla ya mshindi wa mwaka huu kutangazwa vinara hao walikuwa wameshapokezana mara 10 huku kila mmoja akiwa ameibeba mara tano na wote walikuwa wakipewa nafasi ya kunyakua tena. Hata hivyo, baada ya kushindwa kutamba kwenye michuano ya fainali za Kombe la Dunia ndicho kilichowapa nafasi nyota wengine kuchomoza na mmoja wao Modric akapata nafasi ya kuwagalagaza.

3.Fainali za Kombe la Dunia Pia kabla ya juzi kutangazwa mshindi, Modric alikuwa ameshajijengea mazingira ya kutwaa tuzo hiyo ya Ballon d'Or kufuatia mafanikio ambayo aliyapata katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA msimu uliopita.

Mbali na hilo pia kiwango alichokionesha wakati wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka huu nchini Urusi nayo ilikuwa ni silaha tosha kuwafunika mahasimu wake. Akiwa ametwishwa jukumu la unahodha, staa huyo aliweza kufunga mabao mawili muhimu na kutoa ‘asisti’ moja yaliyoisaidia timu yake kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo kutinga hatua ya fainali.

4. Kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Kuna vitu vingi ambavyo vilimsaidia Modric katika safari yake ya kutwaa tuzo hiyo ya Ballon d'Or kwa mwaka huu na mojawapo ni ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Msimu uliopita Modric alikuwa hakamatiki katika safu ya kiungo akiwaunganisha mabeki na washambuliaji, kutuliza kasi ya mchezo, kutoa pasi murua sambamba na kuimarisha kiwango cha uchezaji kwa timu yake. Raia huyo wa Croatia aliumaliza msimu huo akiwa mmoja kati ya wachezaji walioonesha kiwango cha hali ya juu kilichoiwezesha Real Madrid kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mara tatu mfululizo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.