SI VIBAYA KUANZA UPYA,

KAA MBALI NA MAUMIVU

Bingwa - - MAKALA -

KUNA jambo kila mtu anatakiwa kuliamua kwa sababu ya amani na furaha ya maisha yake.

Kama upo katika uhusiano wa amani na furaha, unatakiwa kuamua kuwa bora zaidi ili amani na furaha yako iweze kuendelea.

Ni vigumu sana kuendelea kufurahishwa na mwenzako ikiwa unafanya matendo ya kumuudhi na kumuumiza.

Kuanzia leo, kama unataka kuona amani na raha uliyo nayo katika uhusiano wako inaendelea, kuwa mtu bora na mwafaka katika maisha yake.

Kwa kila kitendo unachotakiwa kufanya hakikisha unakifanya kwa namna inayotakiwa, ila pia kwa kila jambo unalotakiwa kukaa nalo mbali hakikisha unaliepuka ili uweze kumfanya kuwa na amani na utulivu wa nafsi.

Kwa maendeleo ya furaha yako, amua kumpa amani na raha mwenzako. Katika uhusiano, raha huwa ni kitu cha kusababishwa hasa mkiwa mnapendana.

Yaani kama unataka akupe raha na amani, inabidi umsababishe yeye kuwa na amani na furaha. Kiasili, binadamu ana tabia ya kutaka kulipiza kisasi.

Kama ukimfanyia ujinga leo, kuna hatari hata yeye kukufanyia ujinga kesho. Hali hii kwa wengi inaweza isionekane leo au kesho.

Wewe kila siku unaweza kumfanyia mwenzako matendo yasiyostahili na ukadhani hajali ila tambua kuna kitu kitakuja.

Siku atakayosema hapana na kila kitu katika maisha yako kitabadilika. Kwa mahitaji ya amani yako ya kesho, anza kumpa amani yeye leo.

Wengi wenye furaha na amani katika maisha yao ya kimahusiano walianza kutoa amani kwa wenzao kwanza.

Walikuwa wapole na wenye maneno mazuri, wakawa bora katika nyanja za kimahusiano na hatimaye wamewafanya wenzao waanze kuwatazama katika namna inayotakiwa.

Huna amani katika uhusiano wako? Kila siku kwako ni ugomvi na karaha, hakuna thamani wala maana ya kuwa katika uhusiano?

Umejaribu kila kitu kwa ajili ya kuleta amani katika uhusiano wako umeshindwa? Umekuwa mpole, ukawa mnyenyekevu, ukajifanya pia mjinga ili ajue thamani na hadhi yako katika maisha yake ila ameendelea kuwa tofauti?

Kataa kuendelea kuwa katika uhusiano wa namna hiyo! Kila mmoja anahitajika kuwa na mtu anayempenda na kumheshimu. Amjali na amthamini kwa kiwango cha kipekee na namna iliyo bora.

Mapenzi hayapimwi kwa maneno, ili iwe kweli anakupeda inabidi aoneshe kwa matendo na wakati mwingine kuthibitisha kwa kauli.

Sasa kama anakutesa na kila siku anakusababishia maumivu ni kwa namna gani tuseme anakupenda? Kuwa makini.

Anza kumsoma mwenzako vizuri. Chunguza matendo yake kwa kina kuujua ukweli. Ndiyo, unampenda sana.

Huenda akawa ni mtu wa ndoto yako, ila jiulize ni kwa namna gani uhusiano wako utaleta maana kama ukiwa na mtu asiyekupenda?

Na kwa namna gani unaweza kupendwa mahali unapoteswa, unadharaulika na kunyanyasika?

Kataa maumivu katika nafsi yako, karibisha furaha na amani. Daima huwezi kuwa na amani kwa mtu asiyekujali wala kuthamini chozi lako.

Huwezi kuona raha na furaha ya maisha ikiwa unanyanyasika na kudharaulika. Ni ngumu kuachana na mtu unayempenda, ila pia kuendelea kuishi na mtu unayempenda halafu yeye hakupendi maana yake ni kukubali maumivu na karaha.

Kama ulivyokuwa humjui, anza hatua za kumsahau katika maisha yako leo. Kuwa naye mbali na kukudhoofisha kiakili ila pia anafanya usipate nafasi ya kuwa na mtu atakayekujali na kukuthamini.

Yupo wa aina hiyo, achana na mawazo kuwa hakuna kama huyo. Labda, hakuna atakayekutesa kama huyo ila yupo bora zaidi na mwenye heshima na hadhi zaidi ya huyo.

Kubali haya maumivu ya muda mfupi ya kuachana naye. Wengi ni waoga kukubali haya maumivu ya muda mfupi na matokeo yake wanakuwa na maumivu ya muda wote.

Amua kuwa na furaha leo, maisha yako ni yako. Ni wewe unaweza kuyapa thamani na ni wewe unaweza kuyafanya yasiwe kitu.

Anza kila kitu kwa ajili ya kuleta furaha katika maisha yako. Hakuna raha ya kuishi kama huna amani.

Sasa ni kwanini fulani akuondolee raha ya maisha ikiwa mapenzi ni kwa ajili ya kufurahia maisha?

Kubali kuumia kwa muda fulani ili utengeneze furaha na amani ya muda mrefu katika maisha yako. Kuanza upya si ujinga ila ni kuamua kubadili upepo wa miasha yako.

Wewe ndiye mwenye dhamana na maamuzi ya mwisho katika maisha yako. Amua sasa kuwa na aina ya maisha unayotaka.

Mazoea yako na fulani yasikufanye ukadhani ni bora ufe kwa kuvumilia mateso, karaha na manyanyaso yake. Binadamu ni kiumbe bora sana. Heshimu suala hilo.

Japo unampenda sana ila kama hakujali, hakuthamini na zaidi ya yote anatumia kigezo cha wewe kumpenda kukupa mateso makali, mwache aende.

Inauma kupoteza ila tambua ni vema ukawa huna kisha ukawa unaumia kuliko kuwa naye na ukawa unaumia zaidi.

Akiondoka utapata wa kuziba pengo lake. Na huenda akawa bora na wa thamani zaidi yake, mifano iko mingi.

Wapo waliodhani hawawezi kupata wenzi bora na kuamua kuvumilia mateso yasiyofaa ila baada ya kufanya maamuzi katika maisha yao, leo wako na watu wenye kuwapa raha, amani na starehe kubwa katika maisha yao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.