BIASHARA UTD WATOA UFAFANUZI SAKATA LA KOCHA

Bingwa - - HABARI ZA KITAA - NA DAMIAN MASYENENE, MWANZA

WIMBI la kufanya vibaya katika Ligi Kuu Tanzania Bara limeendelea kuisakama timu ya Biashara United ya mkoani Mara, ambayo pia inakabiliwa na janga la kukimbiwa na kocha wake mkuu, Hitimana Thierry, kutokana na madai ya mshahara wa miezi mitatu.

Biashara iliyocheza michezo 14 na kushika nafasi ya 19 ikishinda mmoja, sare saba na kufungwa sita, Jumapili itamenyana na Yanga katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu ya Biashara ambayo huu ni msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu, mwishoni mwa wiki iliyopita ilifungwa mabao 2-1 na Lipuli FC, ambapo kocha wake, Hitimana, hakuwepo benchi na kwa mujibu wa uongozi wa klabu hiyo atakosekana dhidi ya Yanga.

Inadaiwa kwamba kocha huyo raia wa Rwanda yupo nchini kwao kutokana na kuidai klabu hiyo mishahara ya miezi mitatu, ambapo anasubiri kulipwa fedha zake ndipo arejee mjini Musoma.

Akizungumza na BINGWA, Mwenyekiti wa Biashara United, Seleman Mataso, alithibitisha kuwa klabu hiyo inadaiwa na wachezaji pamoja na benchi la ufundi, lakini akaeleza kwamba hiyo si sababu ya kocha wao kutoonekana katika mechi kadhaa za Ligi Kuu.

Aidha, alifafanua kuwa Hitimana amepewa ruhusa ya kupumzika kwa muda wa wiki mbili na madaktari kutokana na kusumbuliwa na maradhi, hivyo anatarajiwa kuungana na timu mara itakaporejea kutoka jijini Dar es Salaam baada ya mechi dhidi ya Yanga.

“Timu ipo jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi ya Yanga, kocha alikuwa likizo na tayari amerejea lakini kinachofanya asiwepo kwenye benchi la ufundi ni maradhi, madaktari wamemwambia apumzike,” alisema Mataso.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.