Mhungula, Majengo FC zatoka sare

Bingwa - - HABARI ZA KITAA - NA PASCHAL MALULU, KAHAMA

TIMU ya Mhungula FC na Majengo FC za mjini Kahama, juzi zilishindwa kutambiana baada ya kulazimishana sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na Ligi Daraja la Tatu Mkoa wa Shinyanga, itakayoanza Desemba 8, mwaka huu.

Akizungumzia maandalizi ya timu yao, Katibu Mkuu wa Majengo FC, Taratibu Misana, alisema mchezo huo ulikuwa maalumu kwa ajili ya kusoma uwezo wa wachezaji wapya waliojiunga na kikosini.

"Sehemu kubwa ya wachezaji wa kikosi chetu ni wale waliokuwepo awali, kwani kocha alisisitiza kusajili wachezaji wengi ni kuharibu muunganiko wa timu, hivyo tumeongeza wachache kuziba pengo katika safu ya ushambuliaji na viungo," alisema.

Aidha, Misana alisema wameshasajili wachezaji wanne akiwemo mmoja kutoka visiwani Zanzibar ili kuongeza nguvu na usajili huo umefanywa kukidhi mahitaji ya benchi la ufundi.

Kwa upande wa kocha msaidizi wa Mhungula FC, Uchumi Abdallah, alisema matokeo ya sare waliyopata yametokana na baadhi ya wachezaji wao kushindwa kufika uwanjani baada ya kukosa usafiri.

"Timu ipo vizuri na ukiangalia tulikuwa tunaanza kufunga wanarudisha, wapinzani wetu kwenye ligi ya mkoa wajipange maana tupo vizuri zaidi ya wanavyotuchukulia, malengo yetu ni kushinda mechi tatu za mwanzo kwenye makundi,” alisema Abdallah.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Shinyanga (Shirefa), Bevin Kapufi, ligi ya mkoa msimu huu inatarajiwa kuanza wikiendi hii ikishirikisha timu 16 zitakazopangwa katika makundi matatu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.