Tajiri wa masikini

Bingwa - - HADITHI - Nini kitaendelea? Usikose kesho.

Ilipoishia Jumatatu asubuhi nilisafiri hadi Port Villa, nilifika kwenye nyumba yangu iliyoko mtaa wa Vaganoa nikatulia na kuanza kufikiria kazi yangu ya usiku ya kufukua makaburi. Wakati huo nilikuwa nikiwaza namna ya kutekeleza ahadi ya Theresa ya kurudi nyumbani kwao kwenda kuendelea na kazi yangu ya utunzaji wa bustani

SASA ENDELEA

Suala hilo liliniumiza sana kichwa kwa sababu nilikuwa nimemwahidi kurudi, wakati huo huo pia nilikuwa nikihitaji kusimamia msimamo wangu ule ule wa kutorudi kwa tajiri Alexender Rugoa.

Sikuhitaji mkono wa Theresa pekee unisaidie kututoa sisi Wapache katika umasikini uliotukuka. Kwa sababu nilikuwa nikihitaji mambo yaende haraka sana ndio maana niliamua kuchagua kazi hiyo hatari, nikiamini msaada wa Theresa hautakuwa wa haraka sana kama hatua niliyochukua.

Niliamua kufikia uamuzi wa kuvunja ahadi niliyomwahidi malaika Theresa na kuamua kusubiri usiku uingie ili niende makaburi ya Wazawa kwenda kufukua kaburi la tatu. Mawazo yangu ya hatari yalikuwa ni kuhakikisha makaburi yote ya Wazawa hayabakiwi na hata mali wala pesa yoyote.

Nilijisemea kuwa lazima nifukue kila kaburi lililopo juu ya ardhi ya nchi yote ya Canibella hasa ya jijini Port Villa. Usiku wa siku hiyo ulipoingia, nilibeba vifaa vyangu kama kawaida na kuelekea makaburini, ambako siku zote hakukuwa na walinzi. Wahai walikuwa hawafikirii wala kuamini kama kuna watu wanaoweza kuiba mali za makaburini. Ni kweli hakukuwa na majambazi wa aina hiyo kutokana na jinsi kila Mhai alivyokuwa akilichukua suala hilo la kumzika marehemu na mali zake lilivyoheshimika kwa watu wa kabila hilo.

Nilifika makaburini na kutafuta kaburi zuri alilozikwa mtu tajiri na kuanza kuchimba. Kazi hiyo ilikuwa inanihitaji nguvu na haraka kubwa kutokana na ugumu wa kazi yenyewe. Baada ya kama dakika 45 hivi nilikuwa nimevunja ukuta wa kaburi na kuingia kaburini. Uzuri na urahisi kwangu ulikuwa ni kutofungua majeneza yenyewe ya marahemu kwa sababu mali hizo zilikuwa zikiwekwa nje ya jeneza.

Kama kawaida ndani ya kaburi hilo niliziona pete za dhahabu, bangili za almasi ikionyesha marehemu aliyezikwa humo alikuwa ni mwanamke, pesa nyingi zilikuwa kwenye mfuko na nje. Sikuacha kitu chochote nilibeba kila kitu na kuvitoa nje ya kaburi.

Baada ya kutumia ujuzi wangu kwa kuurudishia mchanga katika shimo nililochimba, niliondoka makaburini kwa umakini mkubwa hadi nilipofika nyumbani kwangu. Kama kawaida nilimshukuru Mungu kwa kazi hiyo kabla ya kuhesabu pesa na kupiga tathmini ya mali za madini.

Siku hiyo nilikuwa nimepata pesa na mali kama zile nilizoiba kwenye kaburi za marehemu Tino Makenzi, hakika nilizidi kuona mwanga wa kuvifanya vitongoji vyetu vya Adorra na Katanga kuwa sehemu ya kuishi mtu yeyote yule.

Kesho yake nikiwa hapo hapo mafichoni pangu nyumbani kwangu, nilikuwa nikifikiria namna ya kupata soko la nje ya nchi kwa ajili ya kuziuza mali hizo. Mawazo yangu yalinipeleka Kaskazini mwa nchi yetu katika nchi ya Gazar, niliona nikienda kufanyia biashara hiyo huko, sitakuwa matatani kwa sababu sitakamatwa.

Ilikuwa ni ngumu kuuza mali hizo hapo nikihofia kugundulika, ukizingatia mimi nilikuwa ni Mpache nisingeweza kufanya biashara hiyo, kwa sababu jamii nzima ya Wahai wanajua kuwa hakuna Mpache yeyote anayemiliki dhahabu au almasi wala kitu chochote cha thamani ya madini.

Mwanzoni nilikuwa nikifikiria kufanya biashara hiyo kwa wageni wanaoingia nchini humo, lakini baadaye niligundua kuwa wageni hao wangeweza kukamatwa katika njia za kutokea nje ya nchi kama vile kwenye viwanja vya ndege, treni au mabasi, maana pete na vito vingine vya thamani vya Canibella vilikuwa ni vya kipeke. Hivyo kama wageni hao wangekamatwa, niliona kabisa kuwa basi wangenitaja mimi kama mhusika mkuu wa biashara hiyo.

Jioni ya usiku huo tena nilikwenda makaburini na kufukua kaburi lingine, nilirudi na mali nyingine nyingi, hakika nilizidi kuona utajiri unaokwenda kunisogelea hivi karibuni. Niliziweka mali hizo katika lile shimo la ndani huku pesa nikiziweka katika sanduku maalumu.

Jioni ya saa 10 nilifunga mlango wangu na kuondoka, nilipita sokoni kwa Rahimu ambapo alifurahi sana kuniona. Ila aliniuliza nilikuwa nimekuja lini, nilimwongopea nikimwambia kuwa nilikuwa nimekwenda nyumbani kwa Tajiri Alexender Rugoa.

Nilimweleza jambo lililomfanya ashangae sana la msichana mzuri Theresa kufika kwetu Adorra. Hakuniamini mara moja, ilinilazimu kumwaminisha sana hadi alipokubaliana na mimi hapo baadaye. Aliniambia kuwa bahati ilikuwa imeniangukia mimi, akisema kuwa maisha mazuri yananifuata.

“Hakika una bahati Vanuell, mimi mwenyewe sikuwahi kufika kwenu Adorra lakini huyo msichana amefika. Inaonyesha ni namna gani anavyokujali,” aliongea Rahimu kwa msisitizo sana. Nilitabasamu na kumwambia.

“Rahimu wewe hukuwa na muda tu wa kufika kwetu ila siku moja niliamini ungefika, kati ya watu ninaowaheshimu katika dunia hii wewe ni namba moja, umenitoa mbali sana tena mbali.”

“Usiseme hivyo Vanuell mbona nimefanya ya kawaida sana.”

“Hapana Rahimu, wewe ni zaidi ya ndugu ni muhimu sana kuliko hata Theresa kwa sababu bila wewe nisingekutana na hata huyo msichana.”

Baadaye Rahimu aliniambia jambo lililonishtua sana, nilibaki namtolea tu macho.

“Sikiliza Rahimu mimi naamini huyo Theresa anakupenda yaani anahitaji uwe mtu wa muhimu moyoni mwake, pengine uje umuoe.”

Aliposema hivyo nilikaa kimya kidogo nikiyatafakari maneno hayo, kisha nikacheka sana, maana niliona Rahimu anaongea utani uliotukuka.

“Unacheka nini sasa?” aliniuliza.

“Kwa sababu unaongea kitu kisichowezekana hapa chini ya jua,” nilimjibu.

“Kwanini unasema hivyo Vanuell, hutaki kuamini jambo hilo?” “Rahimu mimi nipendwe na Theresa kimapenzi, mimi Vanuell Banguwi?” Nilimuuliza kwa mshangao mkubwa nikijishika kifuani.

“Kwanini isiwezekane, wewe ni kijana mzuri wa sura, mpole una hekima na una kila kitu cha kumvutia mwanamke,” aliniambia. Haraka nilimuuliza. “Kama ni hivyo kwanini Rumia aliniacha?”

Alinicheka kidogo kisha akasema.

“Kwa sababu alikuwa akihitaji maisha mazuri, alikuwa akihitaji mtu mwenye pesa.”

“Sasa unadhani Theresa atanipendea nini mimi sina pesa natokea eneo kama lile la Adorra?”

“Sikiliza Vanuell msichana tajiri haitaji pesa kutoka kwako kwa sababu tayari anazo, anachohitaji kwako ni mapenzi tu.”

“Pamoja na hayo Rahimu ni jambo la fikra za abunuwasi Theresa kunipenda mimi, haitawezekana kamwe, hivi unadhani amekutana na wanaume wangapi hapa nchini na hata nje ya nchi?” nilihoji.

“Usiwe na fikra hizo Vanuell mapenzi hayachagui mtu na mtu bali moyo wako au wake ndio una nguvu ya maamuzi.”

Nilimpuuzia Rahimu kwa fikra zake hizo zisiso za ukweli. Kwa sababu mimi mwenyewe hata siku moja sikuwahi kufikiria wala kuhisi Theresa anaweza kunipenda mimi, niliamini atanipenda kama rafiki yake tu na si vinginevyo. Hata kama moyo wangu ulimpenda malaika huyu wa bustanini nilitambua wazi kabisa uwezo wa kumpata sikuwa nao hata kidogo. Nilijiona mimi na yeye hatuendani kabisa kwa sababu hadhi aliyokuwa nayo mbele yangu ilikuwa ni kubwa kulinganisha na yangu. Sikustahili kabisa kuwa na mahusiano ya mapenzi na kiumbe huyu wa tajiri Alexender Rugoa.

Baadaye nikiwa namuaga Rahimu alikuja mke wake hapo sokoni, aliponiona mimi hakunisalimia alibaki amesimama nje ya banda la biashara la mumwe, lakini mimi nilijipendekeza kwa kumsalimia.

“Shemeji za siku nyingi karibu ndani.”

Hakunijibu zaidi aliendelea kutazama watu wengine wanaopita katika soko. Kwa hasira Rahimu alimuuliza.

“Mke wangu ina maana humwoni Rahimu, hausikii salamu yake, mbona una tabisa mbaya sana wewe?”

“Nina haraka naomba unipe mzigo mimi niende nyumbani,” alijibu mke wake kwa sauti ya nyodo.

Aliamua kuingia mwenyewe na kuchukua mfuko uliokuwa chini ya meza na kuondoka haraka pale eneo la soko la Rahimu, akimwacha mumewe na hasira kubwa. “Wakati mwingine unaweza ukajuta kwa nini ulioa mke wa namna hii,” aliongea Rahimu.

“Usiseme hivyo Rahimu cha muhimu ni kwamba mnapendana hayo mengine ni tabia tu,” niliongea.

“Hapana Rahimu huyu amezidi kukudharau, hata kama wewe ni Mpache na yeye ni Mhai si kwa hatua hii anayofikia yeye.”

“Usijali Rahimu wala usimchukie mkeo kwa ajili yangu tu yeye ni wako wa maisha, kunichukia mimi hakuwezi kutoa upendo wenu,” niliongea kwa tabasamu.

Baadaye nilimuaga na kuondoka sokoni ambapo nilikwenda kupanda basi la kuelekea Adorra. Nikiwa ndani ya basi nilikuwa nikifikiria mambo mawili yaliyokuwa yakiniumiza sana kichwa, moja ilikuwa ni kuhusu kurudi kufanya kazi kwa tajiri Alexender Rugoa ili nimfurahishe Theresa, mbili ilikuwa ni njia gani nitakayotumia kusafirisha vito vya thamani kwenda nchi ya jirani ya Gazar.

Sikuwa na majibu hata kidogo, moyo wangu ulikataa kabisa kuuharibu urafiki wangu mimi na Theresa, niliamini furaha yake ilikuwa ni urafiki wetu na kukaa pamoja naye bustanini. Lakini jambo kuu ambalo ilikuwa ni lazima nilitekeleze ilikuwa ni kutafuta njia ya kupitisha vitu vya dhahabu na almasi katika mpaka wa Canibella na Gazar.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.