AUSSEMS ATUMA SALAMU NKANA

Bingwa - - MBELE - NA MWAMVITA MTANDA

WAPINZANI wa Simba hatua inayofuata Ligi ya Mabingwa Afrika ni Nkana FC ya Kitwe, Zambia ambao jana iliwatoa UD Songo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 3-1.

Nkana FC ambayo anacheza aliyekuwa beki wa Simba na Yanga, Hassan Ramadhan Kessy, jana ikiwa nyumbani ilishinda bao 1-0 lililofungwa dakika ya 45 kwa njia ya penalti na Kelvin Mubanga.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems, ametamba atawapiga Nkana kutokana na ubora wa kikosi chake ambacho juzi kiliifumua Mbabane Swallows ya Eswatini mabao 4-0 ugenini wakiendeleza ushindi mnono wa mabao 4-1 waliopata mchezo wa kwanza.

Akizungumza na BINGWA jana, Aussems, alisema tayari ameshaijenga timu yake katika kiwango cha kimataifa, hivyo hana hofu yoyote na timu hiyo.

“Natambua ubora wao, lakini siwezi kulinganisha na timu yangu, Simba ya sasa ni ya kimataifa, inafanya vizuri, matumaini ya kuwafunga Nkana yapo kwa asilimia kubwa sana,” alisema kocha.

Aussems alisema, Nkana wajipange kisawasawa la sivyo wataifunga mabao mengi ya nje na ndani ya uwanja na kwamba hataki mchezo na anachokifanya zaidi ya kutaka ubingwa.

“Tungeweza kuwafunga Mbabane hata mabao mengi, lakini kuna mambo madogo tu ya kurekebisha kwa mastraika wangu, lakini nimepata nguvu zaidi kwa juhudi walizozifanya na sasa nimerudi na mipango mipya,” alisema Aussems.

Aidha, kocha huyo alisema ushindi kwake ni mwendelezo wa historia kwa kuwa hajawahi kuondoka katika timu yoyote na kuacha matokeo mabovu.

Aussems aliongeza kuwa jambo ambalo lilikuwa linampa tabu zaidi ni mfumo mpya ambao alikuja nao ndani ya kikosi hicho, ikiwa baadhi ya wachezaji walikuwa wanashindwa kukopi kwa haraka, lakini kwa sasa wote wamefanikiwa kuendana nao.

Endapo Simba itaiondoa Nkana FC, itakuwa imefuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo droo imepangwa kufanyika mapema mwakani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.