YANGA KUIVAA BIASHARA UTD ASFC, ZAHERA ACHEKELEA

Bingwa - - HABARI/TANGAZO - NA MAREGES NYAMAKA

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga sasa watavaana na Biashara United katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), baada ya droo ya michuano hiyo kuchezeshwa jana jijini Dar es Salaam.

Michezo yote 16 inatarajiwa kuchezwa kati ya Januari 25 na 28 mwaka huu, kabla ya mwendelezo wa raundi ya 16 bora kuelekea hatua ya robo fainali ambayo pia droo yake ilichezeshwa.

Yanga wataendelea kubaki katika Uwanja wa nyumbani wa Taifa, Dar es Salaam, kama ilivyokuwa katika hatua iliyopita ambapo walikutana na Tukuyu Stars ya jijini Mbeya na kushinda mabao 4-0.

Kikosi cha Jangwani kinachonolewa na kocha, Mwinyi Zahera, kitaingia uwanjani kikiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya wapinzani wao kutokana na Desemba mwaka jana kuwafunga mabao 2-1 katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumzia mechi hiyo, Zahera alieleza kuwa wana nafasi kubwa ya kusonga mbele katika hatua inayofuata kwani anaamini wachezaji wake wanatambua umuhimu wa mchezo wenyewe, lakini pia wanawafahamu wapinzani wao.

“Haya ni mashindano ambayo tunayapa nafasi kubwa, ila tunahitaji maandalizi na kuweka dhamira ya dhati, tunajua wapinzani wetu watajiandaa vizuri lakini hatuna wasiwasi na hilo,” alisema.

Katika mechezo mingine ya FA, mabingwa watetezi, Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Majimaji, Azam itaikaribisha Pamba SC ya jijini Mwanza, huku Coastal Union wakisafiri ugenini kuifuata Katoyasa FC katika Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Kagera Sugar watamenyana na Mbeya Kwanza, KMC itaivaa Pan African, Lipuli watawakabili Polisi Tanzania, Singida United wataikaribisha JKT Tanzania, wakati Mbeya City wakiumana na Mashujaa katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Pia African Lyon itachuana na Friends Rangers, Might Elephant watavaana na Namungo FC, Dar City wataonyeshana kazi na Cosmo Politan wakati Boma wakicheza na Reha FC.

La Familia wao watawafuata Alliance FC wakati Transits Camp wakichuana na Dodoma FC.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.