Gwasa FC yaendelea kuwapa raha mashabiki

Bingwa - - HABARI - NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

TIMU ya Gwasa FC imeendelea kuwapa raha mashabiki wake, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya New Dundee United katika mchezo wa Ligi ya Mkoa wa Dodoma, uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini hapa.

Kwa matokeo hayo yameifanya Gwasa kufikisha pointi 10 baada ya kucheza michezo minne ikishinda mitatu na sare moja na kuongoza katika Kituo cha Dodoma Mjini.

Akizungumzia matokeo hayo, Mshauri wa ufundi wa timu hiyo, Juma Ikaba, alisema malengo yao ni kutetea ubingwa wao.

Ikaba alisema kwa sasa wamewapa nafasi ya kucheza wachezaji vijana ili kuonesha vipaji vyao.

“Tumewapa nafasi wachezaji vijana, wameonesha wanaweza, Mungu akipenda tutacheza hatua ya sita bora na kuuwakilisha tena Mkoa wa Dodoma katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa,” alisema Ikaba.

Katika mchezo mwingine, timu ya Mji Mpwapwa ilifanikiwa kuichapa bao 1-0 Maskani katika mchezo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Amani wilayani Kongwa.

Timu ya Ntyuka iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Chinyasungwa, uliochezwa kwenye uwanja huo wakati Magereza na Mkonze zilitoka sare ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Sabasaba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.