Januari inakutoa jasho? Wazee wa kubeti tunailegeza kwa mkeka huu

Bingwa - - IJUMAA SPESHO -

NI Januari. Hakuna asiyetambua ugumu wa mwanzoni mwa mwaka. Mambo yanakuwa mengi balaa. Mara watoto walipiwe ada ya shule, mwenye nyumba anataka kodi yake na vikorombwezo kibao.

Kama unasumbuliwa na moja kati ya hayo, mbona ipo njia rahisi tu ya kukufanya uione Januari kama miezi mingine tu! Yani usione tofauti kati yake na Desemba, Novemba, Septemba, n.k.

Cha kufanya, chukua karatasi na peni yako na kisha fuatisha mkeka huu, halafu beti. Kutokana na dondoo za mechi hizi, huenda ukawa mmoja kati ya watakaoanza kuifurahia Januari.

WEST HAM V ARSENAL

Hao ni wapinzani wakubwa jijini London kwani wakati Arsenal ikiwa na maskani yake Kaskazini, West Ham wao wanatokea Magharibi inakopatikana pia Chelsea.

West Ham wanashika nafasi ya 10 wakiwa na pointi 28 na wanakutana na Arsenal ya tano kwenye msimamo kwa pointi zake 41. West Ham ndiyo timu iliyopoteza mechi nyingi za Ligi Kuu dhidi ya Arsenal (29).

Mbaya kwa Gunners ni kwamba, kocha wao, Unai Emery, hajashinda ugenini dhidi ya Manuel Pellegrini anayeinoa West Ham kwa sasa.

Isisahaulike pia, katika mechi sita ambazo Emery amekwenda ugenini kukutana na Pellegrini, amepigwa nne na kutoa sare mbili.

Utabiri: West Ham 1-3 Arsenal

BRIGHTON V LIVERPOOL

Brighton wanaoshika nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu walizimaliza dakika 90 za mchezo wao wa Ligi Kuu uliopita kwa sare ya mabao 2-2 na West Ham United. Liver wanarejea wakiwa na kumbukumbu ya kutandikwa mabao 2-1 na Man City.

Kibarua walichonacho Brighton ni kwamba Liver hawajapoteza michezo miwili mfululizo tangu walipofanya hivyo mwaka 2015 wakiwa chini ya kocha Brendan Rodgers.

Tukirejea katika historia, mitanange iliyopita kati ya timu hizo ni 28, Liver wakiibuka na ushindi mara 16 na kufungwa minne tu.

Utabiri: Brighton 0-2 Liverpool

CHELSEA V NEWCASTLE

Katika mechi 23 walizocheza nyumbani dhidi ya Newcstale, Chelsea wamepoteza moja tu, wakashinda 16 na kutoa sare sita. Kichapo chenyewe ni cha mwaka 2012 wakati Blues wakiwa chini ya kocha Roberto Di Matteo.

Safari hii, Blues wanaonolewa na Maurizio Sarri, wanataka kuendelea kuwamo ‘top four’ baada ya kuikosa msimu uliopita na wababe hao wa jijini London wanashika nafasi ya nne, huku Newcastle wakiwa ya 15.

Habari mbaya kwa Newcastle ni kwamba, hawajashinda mchezo wowote ugenini kati ya 12 waliyokutana na vigogo sita wa Ligi Kuu.

Takwimu zinasema ni mechi 164 zilizowahi kuwakutanisha wakongwe hao wa soka la England, ambapo Chelsea wameshinda 72 na kupoteza 53.

Utabiri: Chelsea 3-0 Newcastle

LEICESTER CITY V SOUTHAMPTON

Wenyeji Leicester wanarejea wakiwa na maumivu kwani walifungwa mabao 2-1 katika mchezo wao uliopita wa Kombe la FA dhidi ya Newport County. Hata hivyo, kasi yao kwenye ligi si mbaya kwani wameshinda mechi tatu kati ya nne zilizopita.

Southampton wanaoshika nafasi ya 18 kwenye msimamo, nao wana nguvu ya kutosha baada ya suluhu waliyoipata nyumbani kwa Chelsea katika mtanange wa mwisho pale Stamford Bridge.

Utabiri: Leicester 2-1 Southampton

CRYSTAL PALACE V WATFORD

Palace watashuka uwanjani kutafuta ushindi wao wa tatu mfululizo kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu, lakini haitakuwa rahisi mbele ya ‘wabishi’ Watford, ambao mchezo wao wa mwisho walitoka sare ya mabao 3-3 na timu nyingine ngumu, Bournemouth.

Wanachotakiwa kukijua mashabiki wa Palace ni kwamba, Watford wamepoteza mechi moja tu kati ya tatu walizocheza ugenini katika siku za hivi karibuni.

Rekodi zinazonesha kuwa katika mechi 118 zilzopita kati ya timu hizo, Palace wametamba mara nyingi kwa kushinda mechi 49 na kupoteza 42, huku nyingine 27 zikiamuliwa kwa matokeo ya sare.

Utabiri: Palace 2-1 Watford

BURNELY V FULHAM

Ni vita ya timu zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja. Iko hivi, Fulham wanashika nafasi ya 19 kwa pointi 14 walizonazo, wakiizidi nane tu Burnely inayokamata nafasi ya 16.

Ukiiamini Fulham katika mkeka wako, tambua kuwa imeshinda mechi tatu tu kati ya 21 zilizokwishachezwa na kila timu msimu huu.

Kabla ya mchezo wa kesho, timu hizo zimeshawahi kuvaana mara 95 na ni Burnely ndiyo inayoongoza kwa kushinda, ikiwa imeitambia Fulham mara 45 na kuchezea vichapo 39.

Utabiri: Burnely 2-1 Fulham

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.