Azam, Simba kitaeleweka Mapinduzi Cup

Bingwa - - MBELE - NA SAADA SALIM, ZANZIBAR

MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Azam, leo watamenyana na KMKM katika nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, wakati Simba watakutana katika nusu fainali nyingine dhidi ya Malindi SC.

Azam wametinga hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare moja katika Kundi B na kukaa kileleni, wakifuatiwa na Malindi.

Kwa upande wa Simba wao walishinda mechi zao tatu na kukaa kileleni mwa Kundi A na kufuatiwa na KMKM katika nafasi ya pili.

Nusu fainali ya kwanza kati ya Azam na KMKM itaanza saa 10:00 jioni na ya pili itakuwa ni ile ya Simba na Malindi saa 2:00 usiku Uwanja wa huo wa Amaan, Unguja.

Azam wamekuwa na rekodi nzuri katika michuano hiyo baada ya mwaka jana kuifunga Singida United kwenye mchezo wa fainali ambayo ilikuwa ikinolewa na Hans van Pluijm, ambaye sasa ni kocha wa timu hiyo ya Chamazi.

Pluijm alisema kwa sasa anahitaji kutetea taji hilo kutokana na jinsi ya kikosi chake kilivyo imara, hivyo atahakikisha anarejea na taji hilo Dar es Salaam kwa kuwa anaamini atawafunga KMKM katika mchezo wao huo wa nusu fainali.

“Nimewaona wapinzani na kufanyia kazi mapungufu ya kikosi changu kwa ajili ya kuhitaji kupata matokeo mazuri na kucheza fainali,” alisema Pluijm.

Wakati kikosi cha kwanza cha Simba kikiwa Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura, kikosi cha akiba na wale wa vijana watacheza nusu fainali usiku na Malindi SC.

Akizungumza na BINGWA jana, kocha aliyeachiwa mikoba Simba, Nico Kiondo, amesema amewaangalia wapinzani wake na kuona mapungufu yao, sasa anahitaji kupata matokeo mazuri.

“Malindi ni timu nzuri, nimewaona wakicheza na mechi yao na Azam, nilikuwapo uwanjani, hivyo tayari nimejua naingia na mbinu gani ili kuhakikisha nawafunga wapinzani wangu hao na kucheza fainali ya michuano hiyo,” alisema Kiondo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.