WAARABU WATAPIGWA KWA STAILI HII

Bingwa - - MBELE - NA AYUBU HINJO

Simba wajinoa kwa mipira ya adhabu

Chama akoleza pasi zake za mpenyezo

KOCHA wa Simba, Patrick Aussems, ameendelea kukipika kikosi chake kimbinu kuhakikisha kinaibuka na ushindi kesho dhidi ya JS Saoura ya Algeria.

Simba wanatarajiwa kuvaana na wapinzani wao hao wa Kundi D katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi ambacho kimetinga hatua hiyo ya makundi kwa mara ya kwanza tangu kifanye hivyo mwaka 2003, kilirejea kutoka Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na kuendelea kujifua.

Kocha wa timu hiyo, Aussems kutoka Ubelgiji, alitumia michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi kujiandaa na mchezo huo, lakini jana aliendelea kukiweka sawa kikosi chake katika mambo ya kiufundi.

Katika mazoezi hayo ya jana yaliyoendelea kwenye Uwanja wa Boko Veterani, jijini Dar es Salaam, kocha huyo alionekana akisisitiza viungo na washambuliaji wake kufanya kazi kwa ushirikiano ili kutengeneza nafasi za mabao na kuzitumia.

Aussems alionekana akipiga sana makelele kwa akina Emmanuel Okwi, John Bocco, Meddie Kagere, Clatous Chama, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na Haruna Niyonzima ambao walicheza dhidi ya ukuta wa mabeki wanne uliokuwa na Pascal Wawa, Jjuuko Murshid, Nicolas Gyan na Mohamed Hussein.

Kwa kiasi kikubwa kocha huyo aliwaongoza wachezaji wake kufanya mazoezi ya mbinu ya kuipenya ngome ya ulinzi ya JS Saoura.

"Huwezi kufunga bao kama hutengenezi nafasi, lazima hilo lifanyike na kwa kiasi kikubwa viungo na washambuliaji wangu wamefanya vizuri,” alisema Aussems.

"Kama tutaendelea na kasi yetu tuliyotumia michezo iliyopita dhidi ya Mbabane Swallows na Nkana FC, tutakuwa na nafasi ya kushinda mchezo tena kwa mabao mengi.”

Pia, alifafanua kuwa anazijua vizuri timu zenye asili ya Waarabu kwa kuwa na mbinu nyingi za kutafuta mabao hasa kwa kudanganya waamuzi kwa kujiangusha eneo la hatari, ambapo wapinzani wao hao wamefunga mabao manne na matatu yakipatikana kwa njia ya penalti.

"Nawajua vizuri Waarabu, wakiguswa kidogo watadondoka na kugalagala chini, sisi tumejipanga kwa kila kitu hasa kwa upande wetu jinsi gani tutaweza kushinda michezo yetu yote ya hapa nyumbani," aliongeza kocha.

Hata hivyo, kocha huyo aliendelea na mazoezi hayo huku mara ya pili alipanga vikosi viwili tofauti ambavyo kimoja kilicheza kwa kushambulia na kingine kuzuia.

Naye Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson, atakuwapo uwanjani kuongoza mashabiki wa soka Tanzania kushuhudia mchezo huo. Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara, Dk. Tulia ambaye ni mbunge wa kuteuliwa atakuwa mgeni rasmi wa mchezo huo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.