YANGA WAONDOKA NA MTU ZANZIBAR

Bingwa - - MBELE - NA SAADA SALIM, ZANZIBAR

ZAHERA ACHEKELEA DROO KOMBE LA SHIRIKISHO

UONGOZI wa klabu ya Yanga umeanza kumtolea macho kipa wa Malindi ya Zanzibar, Ahmed Ali, kumrithi Beno Kakolanya, ambaye hadi sasa hatima yake ndani ya vinara hao wa Ligi Kuu Bara haijulikani.

Ali amekuwa na mchango mkubwa kwa timu yake ya Malindi kutinga hatua ya nusu fainali michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea hapa Zanzibar, ambako leo watacheza na Simba.

Akizungumza na BINGWA jana, kipa huyo alikiri kufuatwa na mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye alitaka kufahamu mkataba wake na Malindi.

Alisema kiongozi huyo alimwambia Yanga wapo katika mchakato wa kusaka kipa kwa ajili ya msimu ujao na kumdokeza jina lake litapelekwa mezani mwa kamati ya usajili ili kujadiliwa.

“Huyo kiongozi ambaye jina lake silifahamu alikuja kunieleza wanahitaji huduma yangu kwa msimu ujao na nilimwambia niko tayari kutokana na mkataba wangu na Malindi unakaribia kumalizika,” alisema Ali.

Kipa huyo alisema amebakisha miezi sita kumaliza mkataba wake na Malindi na yuko tayari kusaini na Yanga endapo uongozi wa klabu hiyo utahitaji huduma yake msimu ujao.

Alipotafutwa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, kuhusu Yanga kuhusishwa na kipa wa Malindi, alisema hata yeye anazisikia tu taarifa hizo.

“Hizo taarifa siwezi kuthibitisha kwa sababu mimi mwenyewe pia nazisikia, mpango wa kumsajili msimu ujao kuongeza nguvu ndani ya kikosi cha Yanga,” alisema.

Hafidh alisema amemwona kipa huyo katika mechi ambazo timu yake ya Malindi imecheza michuano ya Kombe la Mapinduzi na kukiri ni mchezaji mzuri anayeweza kuisaidia timu yoyote.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.