Mao, Banda wampa mchongo Zayd

Bingwa - - HABARI/TANGAZO - NA ZAINAB IDDY

WACHEZAJI wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Banda na Himid Mao, wamemtaka kinda wa Azam FC, Yahya Zayd, afanye kazi kwa kujituma na kuonyesha nidhamu ili aweze kudumu katika maisha yake mapya ya kucheza soka la kulipwa.

Zayd amepata dili la kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Ismailia ya nchini Misri, baada ya kufuzu vipimo vya afya na kuingia mkataba wa miaka mitatu mwanzoni mwa mwaka huu.

Akizungumza na BINGWA, Mao, alisema alichofanya Zayd anastahili pongezi kwa kupiga hatua mbele, lakini atambue bado ana kazi kubwa ya kuhakikisha anafanya kile kilichompeleka Misri.

“Nampa hongera kwa kuwa hii ni nafasi nzuri kwake kuonyesha kile alichonacho ambacho kimewavutia Ismailia, lakini ili atimize hili kuna mambo makuu mawili lazima ayaache.

“Kwanza anatakiwa kukua kifikra kwa maana ya kufahamu anakwenda nchi za watu na kule ataiwakilisha Tanzania, pia nidhamu na kujituma ni vitu muhimu katika maendeleo yake ya soka,” alisema Mao anayecheza katika timu ya HYPERLINK "https://www.transfermarkt.com/ petrojet/startseite/verein/10957"Petrojet.

Kwa upande wa Banda anayecheza katika timu ya Baroka FC nchini Afrika Kusini, alisema hivi sasa kila Mtanzania kijana aliyecheza soka anatamani kufika alipo Mbwana Samatta, hivyo ili kumfikia ni lazima kuwa na nidhamu ya kazi.

“Nje ya Tanzania hakuna mpira wa kujuana, kiwango tu ndio kinampa mchezaji nafasi ya kucheza, binafsi namwamini Zayd na natamani siku moja afike pale ambapo wengi tunatamani kufika,” alisema Banda.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.