Ushindi waipa jeuri Prisons Ligi Kuu Bara

Bingwa - - HABARI/TANGAZO - NA SALMA MPELI

USHINDI wa mabao 2-0 walioupata timu ya Tanzania Prisons dhidi ya Mtibwa Sugar, umeanza kumpa jeuri kocha mpya wa kikosi hicho, Adolf Rishard, ambaye amesema kazi ndiyo imeanza.

Rishard alianza kuinoa Prisons hivi karibuni akichukua mikoba ya aliyekuwa kocha mkuu, Mohamed Abdallah ‘Bares’, ambaye alifungashiwa virago kutokana na matokeo mabaya waliokuwa wanayapata katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumzia matokeo hayo, Rishard alisema sasa wameanza harakati za kuhakikisha wanainusuru timu yao isishuke daraja, ambapo kwa kuanza watapambana kujinasua kutoka mkiani.

“Matokeo haya yametusaidia kusogea nafasi moja mbele kwenye msimamo wa ligi, hata hivyo tumejipanga kushinda mechi zilizobaki ili kuinusuru timu kushuka daraja,” alisema Rishard.

Ushindi dhidi ya Mtibwa ulikuwa wa pili kwa Prisons tangu kuanza Ligi Kuu msimu huu, ambapo umeiwezesha kufikisha pointi 15 kutokana na mechi 20 walizocheza.

Mtibwa inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 26 baada ya kucheza michezo 16.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.