KIUNGO YANGA SC AFANYISHWA MAZOEZI MAALUMU

Bingwa - - MISIMAMO RATIBA -

KIUNGO wa Yanga, Juma Mahadhi, amepangiwa programu maalumu ya mazoezi kwa ajili ya kurejesha sehemu iliyofanyiwa upasuaji ili hali yake irudi ya kawaida na kisha kuanza mazoezi ya mpira.

Mahadhi, aliyeumia kabla ya msimu huu wa Ligi Kuu Bara kuanza, alifanyiwa upasuaji wa goti mara mbili Oktoba mwaka jana, baada ya ule wa awali kukosewa.

Akizungumza na BINGWA jana, Daktari wa Yanga, Edward Bavu, alisema nyota huyo anaendelea vizuri na sasa yupo katika mazoezi maalumu kurudisha goti lake katika hali ya kawaida.

Alisema Mahadhi, ambaye yupo nje ya uwanja kwa muda, anaendelea na mazoezi ambapo alianza kwa kutembea bila magongo na sasa anakimbia taratibu ufukweni.

“Kwa sasa sitaweza kusema atakuwa nje kwa muda gani kwasababu jeraha la goti linachukua muda kidogo,” alisema Bavu.

Alisema kutokana na upasuaji mara mbili, nyota huyo hatakiwi kufanya haraka kurejea uwanjani hadi ripoti ya madaktari itakapothibitisha lini anapaswa kuanza mazoezi ya nguvu na kucheza mechi.

Juma Mahdhi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.