Yanga kamili kuivaa Mwadui

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo watakamilisha maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa Mwadui FC katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa kesho Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Bingwa - - MBELE - NA HUSSEIN OMAR

Kikosi hicho kinachonolewa na kocha kutoka DR Congo, Mwinyi Zahera, kitafanya mazoezi hayo ya mwisho kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, jijini Dar es Salaam.

Kesho Yanga watawakaribisha Mwadui FC katika mchezo utakaopigwa saa 1:00 usiku, huku kikosi hicho kikiwa kamili baada ya wachezaji waliokuwa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi kurejea.

Kikosi hicho kiliondolewa kwenye michuano ya Mapinduzi huko Visiwani Zanzibar na kimeendelea na mazoezi yake makali Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam, kuhakikisha kinaendeleza moto wao wa ushindi.

Akizungumza na BINGWA jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kikosi cha timu hiyo kimeingia kambini jana usiku katika Hoteli ya Nefaland iliyopo Manzese kujiandaa na mchezo huo, huku wachezaji wao wote wakiwa fiti.

“Tumeingia kambini tangu jana, kama unavyofahamu kocha wetu amepania kufanya kweli katika mzunguko huu wa pili, ndiyo maana utaona safari hii tumeingia kambini siku mbili kabla ya mchezo, kitu ambacho haikuwa hivyo,” alisema Hafidh.

Alisema kuelekea katika mchezo huo wa kesho, ni wachezaji wawili pekee ndio majeruhi, ambao ni Juma Mahadh na Raphael Daudi na hawana mchezaji anayetumikia adhabu ya kadi tatu za njano katika kikosi chao.

Hafidh alisema katika mazoezi yaliyofanyika jana na juzi kocha Zahera alikuwa na kazi ya kuwafundisha vijana wake namna ya upigaji wa mikwaju ya penalty na faulo kuhakikisha wanazitumia nafasi hizo wakizipata.

“Kikosi kipo vizuri sana, walikuwa wanacheza mechi mazoezi kwa muda wa dakika 100 hadi 120, yote hii ni kwa ajili ya kuwapa pumzi ya kutosha, lakini pia kuwawezesha kuwa fiti katika muda wote wa mchezo wakati wa ligi, ’’ alisema Hafidh.

Pia Hafidh aliwataka wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa sapoti wachezaji ambao wameahidi kufanya makubwa zaidi kuliko michezo iliyopita.

“Mashabiki waje kujaza uwanja kama wanavyofanya mashabiki wa wenzetu upande wa pili, ambao wanaipenda timu hiyo na wanakwenda kwa wingi uwanjani na sisi tunaomba wajitokeze kesho,’’ alisisitiza Hafidh.

Yanga imeendelea kuongoza kwenye msimamo wa ligi ikiwa tayari imejikusanyia pointi 50, huku Azam ikiwa nyuma yao na pointi 40, watani zao wa jadi, Simba wakishikilia nafasi ya tatu wakiwa na pointi 33.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.