Simba SC safi, lakini kazi kubwa ipo mbele

NATOA pongezi nyingi kwa benchi la ufundi la timu ya Simba pamoja na wachezaji kutokana na kandanda safi waliloonyesha katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi, wakati wakicheza dhidi ya JS Saoura kutoka nchini Algeria.

Bingwa - - MTAZAMO MAONI KATUNI -

Simba juzi walianza safari yao katika hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura, hivyo kufanikiwa kuongoza kundi D walilopangwa.

Matokeo haya yamewapa Simba nafasi ya kuongoza kundi lao wakiwa na pointi tatu na mabao matatu, wakifuatiwa na Al Ahly walioshinda mabao 2-0 dhidi ya AS Vita Club ambao hawajaambulia chochote katika mechi ya awali sawa na JS Saoura.

Hakika mchezo wa Simba juzi ulikuwa wa kuvutia pande zote, lakini Waarabu walianza kwa presha kubwa wakiamini wataweza kuvuruga mipango ya Wekundu hao wa Msimbazi.

Simba kwa upande wao walianza kwa kuwasoma wapinzani hao namna wanavyocheza.

Idara ya kiungo ya timu ya Simba muda mwingi iliweza kuutawala mchezo hasa kutokana na ule uwiano wa utatu wa James Kotei, Jonas Mkude na Claotus Chama ambao walipanga vilivyo ili kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Muda mwingi Kotei alikuwa akicheza chini kuwalinda mabeki kutokana na kuamini kwamba, JS Saoura ni wazuri katika kushambulia kwa mipira ya kushtukiza kutoka nyuma kwenda mbele.

Mkude kwa upande wake alikuwa akifanya kazi moja tu ya kuchukua mpira na kumpa Chama aliyekuwa akipandisha mashambulizi.

Katika safu ya ulinzi ya Simba wengi waliamini hakuna beki mwenye uwezo wa kuziba pengo la Erasto Nyoni aliyeumia katika mechi ya Kombe la Mapinduzi, lakini mambo yalionekana kuwa tofauti kabisa na fikra zao. Wengi walidhani hakuna beki mwenye uzoefu na mechi za kimataifa ukimtoa Pascal Wawa, lakini kumbe

Jjuuko Murshid alikuwa anaweza kuimudu vyema nafasi hiyo na kufanya kazi nzuri kipindi cha pili cha mchezo.

Kwa upande wa eneo la ushambuliaji la timu ya Simba, Mganda Emmanuel Okwi, alionekana kuwa mwiba mkali kwa JS Saoura na muda mwingi alikuwa akizunguka uwanjani kutafuta mipira.

Uwezo wa Okwi wa kumiliki mpira na kupiga chenga muda mwingi, uliwafanya mabeki wa JS Saoura washindwe kupanda kushambulia.

Kwa ujumla mchezo wa juzi ulitawaliwa na nidhamu hasa kwa wachezaji wa Simba ambao walikuwa wakicheza kwa tahadhari.

JS Saoura wao waliifuata Simba huku wakitegemea kucheza kwa kujilinda zaidi na kutengeneza nafasi za kufunga jambo ambalo walifeli.

Timu ya Simba ilistahili ushindi dhidi ya JS Saoura kutokana na walivyojipanga kulingana na mbinu walizopewa na Kocha wao mkuu, Patrick Aussems, raia wa Ubelgiji ambaye pia anastahili pongezi nyingi kwa kusuka mipango dhabiti iliyowapa ushindi.

Ushindi huu wa Simba umeonyesha dhahiri kuwa wamedhamiria kurejesha furaha kwa mashabiki wao ambayo ilipotea kwa muda mrefu, baada ya kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Hamasa iliyopo Simba kwa sasa inaonyesha wazi wanaweza kutimiza kile wanachohitaji, lakini jambo la msingi kwao ni kutodharau timu yoyote ambayo watakutana nayo. Licha ya kupata ushindi lakini wanatakiwa kutambua kwamba mechi zilizopo mbele yao ni ngumu zaidi, hivyo kama watabweteka na kuwadharau wapinzani wao watajikuta safari yao inaishia njiani.

Mechi ijayo Simba watasafiri kuifuata AS Vita Club ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), waliotoka kufungwa mabao 2-0 katika mechi yao ya awali ya hatua ya makundi dhidi ya Al Ahly kutoka Misri.

Ninaamini mchezo huo utakuwa mgumu hivyo Simba wanatakiwa kujipanga vyema kabla ya kwenda kuuana na AS Vita Club, kwani mara nyingi mechi za ugenini huwa hazitabiriki.

Hata hivyo, Wekundu wa Msimbazi wataendelea kupambana na ugumu wa michuano hii kwani raundi ya tatu watakwenda kukutana na Waarabu wa Misri, Al Ahly ambao hawana rekodi nzuri kwao.

Hivi sasa Simba wanatakiwa kuzipa uzito mkubwa mechi zote zilizopo mbele yao bila kudharau timu yoyote ambayo wamepangwa kundi moja ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea.

Lakini pia waandae mikakati kabambe ya kuhakikisha wanamaliza kiu ya mashabiki wao kwa kuiwezesha timu kutinga fainali za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.

“ Kwa ujumla mchezo wa juzi ulitawaliwa na nidhamu hasa kwa wachezaji wa Simba ambao walikuwa wakicheza kwa tahadhari.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.