Kocha Mashujaa alia bahati FDL

KOCHA wa timu ya Mashujaa FC, Atuga Manyundo, amesema hawakuwa na bahati ya kuibuka na ushindi dhidi ya Arusha United katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma.

Bingwa - - HABARI - NA GLORY MLAY

Katika mchezo huo, Mashujaa FC walishindwa kuibuka na ushindi baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1.

Kutokana na matokeo hayo, Manyundo amesema wanarudi kujipanga upya ili waweze kupata ushindi dhidi ya Dodoma FC, ambao watacheza Jumamosi wiki hii.

Manyundo alisema katika mchezo wao dhidi ya Arusha United wachezaji wake walitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini walishindwa kuzitumia.

Alisema malengo yao yalikuwa ni kupata pointi tatu, lakini mambo hayakwenda kama walivyopanga katika mchezo huo.

“Mchezo ulikuwa wa ushindani mkali, bahati haikuwa yetu, wachezaji walipata nafasi nyingi za kufunga, lakini hawakuweza kuzitumia, tunaendelea na mazoezi na kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza,” alisema Manyundo.

Mashujaa wanashika nafasi ya 10 katika msimamo wa Kundi B, kutokana na pointi 11 baada ya kucheza michezo 10, wakishinda mitatu, sare mbili, kupoteza mitano.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.