SIMBA WALIOCHEZA FAINALI KOMBE LA CAF 1993 (8)

Bingwa - - HAT-TRICK -

WIKI iliyopita BINGWA Jumatatu lilikukumbusha baadhi ya wachezaji wa Simba waliocheza fainali ya Kombe la CAF na kutolewa na timu ya Stella Abidjan ya Ivory Coast, kwa kufungwa mabao 2-0 mchezo uliochezwa Novemba 29, 1993, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru).

Wafuatao ni mwendelezo wa baadhi ya wachezaji hao ambao baada ya kufungwa mabao hayo walifuta ndoto ya kutwaa zawadi ya magari aina ya KIA waliokuwa wameahidiwa na aliyekuwa mfadhili wao mkuu wa wakati huo, Azim Dewji. 21.THOMAS KIPESE ‘UNCLE THOM’ Winga wa kushoto, Kipese maarufu ‘Uncle Thom’ kama wapenzi wa soka nchini walivyozoea kumwita, ni miongoni mwa wachezaji waliochezea timu ya Simba wakati inacheza fainali ya Kombe la CAF dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast na kukutana na balaa la kufungwa mabao 2-0, huku yeye akicheza safu ya winga wa kushoto.

Mkongwe huyo ambaye ana umbo dogo, alisajiliwa kuchezea Simba katika fainali hiyo akiwa katika orodha ya wachezaji wawili walioongezwa wakitokea klabu ya Yanga. Mwenzake aliyeongezwa naye ni beki Godwin Aswile ‘Scania’.

Kipese wakati wa enzi zake za kucheza soka ya ushindani alisifika kutokana na aina ya ushezaji wake. Akicheza safu ya winga ya kushoto alikuwa na kasi kubwa, chenga za maudhi na uwezo mkubwa wa kupiga krosi.

Mkongwe huyo ambaye pia wakati mwingine alikuwa akichezeshwa beki wa kushoto, alianza kujulikana katika ulimwengu wa soka miaka ya 1980 mwishoni wakati akichezea klabu ya Yanga.

Miongoni mwa wachezaji wa Yanga aliokuwa nao wakati huo ni Juma Pondamali ‘Mensah’, John Alex, Kenneth Mkapa, Godwin Aswile, Said Zimbwe (marehemu), Joseph Machela, Rajab Rashid ‘RR’, Justine Mtekere (marehemu), Athumani China, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’.

Wengine aliocheza nao misimu iliyofuata ni Sahau Kambi (marehemu), Fred Felix ‘Majeshi’, Seleiman Mkati, Stephen Nemes ‘Masajage’, Willy Mtendamema, Jumanne Shengo, Ramadhani Kilambo, David Mwakalebela, Joseph Lazaro, Hamisi Thobias ‘Gagarino’ (marehemu), Issa Athumani (marehemu), Stephen Mussa (marehemu) na John Mngazija (marehemu).

Mkongwe huyo baada ya kuchezea klabu ya Yanga takribani misimu mitano, mwaka 1993 ndipo akiwa na beki Godwin Aswile waliposajiliwa katika kikosi cha Simba kilichocheza fainali ya Kombe la CAF na kukutana na adha hiyo ya kufungwa mabao 2-0, huku yeye akicheza winga ya kushoto.

Miongoni mwa wachezaji aliokuwa nao katika klabu hiyo mpya ya Simba ni Mohamed Mwameja, Rashid Abdallah, Twaha Hamidu ‘Noriega’, George Masatu, Ramadhani Lenny ‘Abega’ (marehemu), Abdul Maneno ‘Mashine’, Hussein Marsha, Malota Soma ‘Ball Juggler, Damian Mrisho ‘Kimti’ na Edward Chumila (marehemu).

22.ABDUL RAMADHANI ‘MASHINE’ Kiungo Ramadhani maarufu Mashine, naye ni miongoni mwa wachezaji waliochezea timu ya Simba wakati inacheza fainali ya Kombe la CAF dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast na kukutana na balaa la kufungwa mabao 2-0, huku yeye akicheza nafasi ya winga ya kulia, lakini baadaye alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na George Lucas ‘Gaza’.

Mkongwe huyo kabla ya kujiunga na Simba na kushiriki michuano hiyo ya Kombe la CAF mwaka huo wa 1993, alitokea klabu ya Kilimanjaro Hotel akiwa na Nico Kiondo ambaye naye alichezea klabu hiyo ya Simba. Hivi sasa Kiondo ni kocha wa timu ya vijana Simba.

Nyota huyo baada ya kujiunga na Simba kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kumiliki mpira, kutoa pasi za uhakika, wapenzi wa klabu ya Simba walimbatiza jina la Mashine wakimaanisha kuwa mkongwe huyo alikuwa mwepesi kuchezea mpira anavyotaka kama mashine.

Baada ya kujiunga na Simba miongoni mwa nyota aliowakuta na kucheza nao katika klabu hiyo ni Mohamed Mwameja, Kasongo Athumani, Rashid Abdallah, George Masatu, Ramadhani Lenny (marehemu), George Lucas ‘Gaza’, Edward Chumila (marehemu), Feroz Teru na Damian Mrisho ‘Kimti’. 23.EDWARD CHUMILA ‘SMILE BOY’ Mshambuliaji mahiri na aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kupachika mabao Chumila, naye ni miongoni mwa wachezaji wa Simba aliyechezea timu hiyo katika fainali ya Kombe la CAF dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast na kupokea kipigo cha mabao 2-0, huku yeye akicheza safu ya ushambuliaji namba 10.

Mkongwe huyo ambaye hivi sasa ni marehemu, kabla ya kujiunga na Simba miaka ya 1980 katikati, aliibukia Temeke katika timu za mitaani.

Baada ya kujiunga na Simba miongoni mwa wachezaji aliowakuta na kucheza nao ni kipa Moses Mkandawile, Adoph Kondo, Twaha Hamidu ‘Noriega’, Kiwhelo Mussa ‘Julio’ na Saulo Jaji (marehemu).

Wengine ni Sunday Juma, Erick Sagala, Kassim Matitu, Ayoub Mzee, Malota Soma ‘Ball Juggler’, Francis Mwikalo, Raphael Paul ‘RP’ (marehemu), Abdallah Mwinyimkuu (marehemu), John Douglas na Mohamed Nyauba.

Pamoja na mkongwe huyo kuwa mahiri katika kupachika mabao, lakini alikuwa katika kikosi cha timu hiyo ya Simba kilichofungwa mabao 2-0 dhidi ya Ivory Coast na kufuta ndoto ya kutwaa zawadi ya magari aina ya KIA waliyokuwa wameahidiwa na aliyekuwa mfadhili wao mkuu, Azim Dewji.

24.FERUZI TERU Winga wa kulia, Teru naye ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa katika kikosi cha Simba kilichocheza fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kuchezea kichapo cha mabao 2-0.

Mkongwe huyu kabla ya kujiunga na Simba msimu wa 1992/1993, alipata umaarufu akichezea timu ya Milambo ya Tabora ambayo ilikuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu).

Miongoni mwa wachezaji aliokuwa nao ni Peter Poka (marehemu), Douglas Muhani, Said Sued ‘Scud’, Dionis Paul, Joub Ayoub ‘Kwasakwasa’, Abbas Mchemba (marehemu) na Quresh Ufunguo.

Mkongwe huyo msimu wa 1993/1994 alinyakuliwa na kusajiliwa na klabu ya Simba na kuwa mmoja wa wachezaji waliosajiliwa kucheza michuano ya Kombe la CAF na kutolewa katika fainali kwa kufungwa mabao 2-0.

Winga wa kushoto, Thomas Kipese (wa pili kutoka kulia waliosimama), akiwa na kikosi cha Simba katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru) mwaka 1993.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.