Mpishi wa mabao ya Okwi atua Simba

Dimba - - News - NA MOHAMED KASSARA

KAMA dili hili litatimia basi Simba itakuwa si tishio Tanzania peke yake, bali Bara zima la Afrika na kila timu itakayokatisha mbele yao inaweza ikaondoka na kipigo kisichoelezeka.

Iko hivi! Wakati wengi wakiamini kwamba safu ya kiungo ya Wekundu hao wa Msimbazi imekamilika vilivyo, wenyewe wapo kwenye mpango wa kumshusha kiungo fundi wa KCCA ya Uganda, Ibrahim Saadam Juma.

Unaambiwa ukimuona Emmanuel Okwi ana ‘shaini’, kwenye timu yake ya Taifa ya Uganda, ‘The Cranes,’ basi ujue mambo yote yamefanywa na kiungo huyu, kwani kombinesheni yao ni ya hatari sana.

Juma ndiye kiungo anayemng’arisha Okwi kwa kumtengenezea mabao katika kikosi cha The Cranes na kumfanya mshambuliaji huyo kuwa moto wa kuotea mbali, baada ya kufunga mabao matatu katika michezo minne ya kufuzu kwa fainali za Afcon.

Mbali na kutengeneza mabao ya Okwi, kiungo huyo ndiye aliyeiongoza KCCA kuwachapa vigogo wa soka la Misri, Al Alhly, katika mchezo wa makundi kwa Klabu Bingwa Afrika msimu uliopita.

Kiungo huyo alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-1 iliyoupata timu hiyo inayomilikiwa na Mamlaka ya Jiji la Kampala, katika mchezo huo ambapo ilipangwa kundi A, pamoja na timu za Al Alhly, Township Rollers ya Botswana na Esperance ya Tunisia.

Kiungo huyo anayetumia mguu wa kulia pia, aliisaidia The Cranes kumaliza nafasi ya tatu katika michuano ya Cecafa iliyofanyika mwaka jana nchini Kenya, akifunga mabao yote mawili katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Burundi.

Akizungumza na Dimba jana, Meneja wa mchezaji huyo, Patrick Gakumba, alisema mbali na Simba, timu nyingine zinazomfukuzia ni Yanga pamoja na Azam FC, lakini wanawapa nafasi kubwa wekundu hao wa Msimbazi.

“Ni kweli nimepokea ofa kutoka timu za Tanzania, Simba, Yanga na Azam, zote zinamhitaji Juma, mchezaji mwenyewe bado ana mkataba na timu yake, lakini wanaweza wakauvunja, naona Simba ndio wamekomaa kumtaka.

“Dau la mteja wangu ni Dola 80,000 (sawa na zaidi Sh milioni 183 za Tanzania), hivyo kama kweli (Simba) wako tayari wazilete wamchukue.

“Ni mchezaji mzuri, ndiyo roho ya timu ya Taifa ya Uganda, ukiona Okwi amefunga ujue kazi yote kaifanya yeye, Waganda wanamuita Sadam Magoli kutokana na uwezo wake, nimeshawaambia kuwa yeyote anayemtaka atoe kiasi hicho na si chini ya hapo, kwa kuwa nina uhakika hawezi kuniangusha,” alisema alisema Gakumba, ambaye ni wakala namba moja Afrika.

Kiungo huyo inadaiwa kuwa, mpira wowote wa faulo uliopo karibu na goli la wapinzani huwa hakosi kufunga bao, ni mbunifu, lakini pia ni mzuri katika kutumia nafasi hiyo, ikimaanisha kwamba Simba watakuwa wamelamba dume kama watamsajili.

USAJILI

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.