Usajili kumpima mrithi wa Manji

Wafanya usajili kimyakimya kuepuka hujuma

Dimba - - Mbele - NA CLARA ALPHONCE

SI unajua kwamba Yanga wapo kwenye mchakamchaka wa kuwapata viongozi wapya, sasa unaambiwa nafasi inayoangaliwa zaidi ni ya mwenyekiti, ambaye atapimwa kwa kigezo cha usajili atakaoifanyia klabu hiyo.

Usajili wa dirisha dogo utaanza Novemba 15, wiki ijayo, ambapo Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ameshaweka bayana kwamba anahitaji wachezaji wane, mmoja kutoka hapa nchini na watatu kutoka nje.

Hivi karibuni Baraza la Michezo la Taifa (BMT), liliwataka Yanga kuitisha uchaguzi kwa ajili ya kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu, ikiwemo ya Mwenyekiti wao wa zamani, Yussuf Manji.

Jana ndiyo rasmi fomu zilianza kutolewa, ambapo nafasi zitakazojazwa ni ya mwenyekiti iliyokuwa ikishikiliwa na Manji, Makamu Mwenyekiti Clement Sanga pamoja na nafasi za wajumbe watano walioamua kuachia ngazi wenyewe.

Ktika uchaguzi huo, nafasi ya mwenyekiti ndiyo imeyotupiwa jicho, kwani Wanayanga wanamtaka mtu ambaye anaijua Yanga vizuri na mwenye uwezo wa kumwaga fedha za usajili, hasa kipindi hiki ambacho wamekuwa kwenye wakati mgumu baada ya Manji kuachia ngazi.

Moja kati ya majina yanayotajwa sana kustahili kuvaa viatu vya Manji na vikamtosha ni Tarimba Abbas, ambaye kwa kiasi kikubwa alifanikisha kumbakisha kikosini beki kisiki Kelvin Yondani.

Mbali na Tarimba, pia wenye Yanga yao wanadai, hata Ridhiwani Kikwete, angefaa, japo mwenyewe amelithibitishia Dimba kwamba, hayupo tayari kugombea kutokana na kubanwa na shughuli zake.

Kwa upande wake Tarimba, ambaye

wengi wanamuamini kutokana na ushawishi alionao, yeye alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote, japo anashukuru kutokana na namna wanachama na mashabiki walio wengi wanavyomkubali.

Kigogo mmoja wa Yanga ameliambia Dimba kuwa, kwa sasa wataendeleza zoezi lao la usajili wa kimyakimya kama walivyofanya dirisha kubwa ili kuepuka hujuma za wapinzani wao.

“Sisi dirisha hili dogo tutafanya usajili kimyakimya, kwani tukiweka mambo yetu wazi wenzetu wanatuzunguka na kutuharibia, kama unakumbuka tulikuwa na mazungumzo na Adam Salamba na alikaribia kusaini, lakini wajanja wakamuwahi.

“Hata Dilunga (Hassan) na Kaheza (Marcel) wote sisi ndio tulioanza nao mazungumzo, lakini baada ya wapinzani wetu kusikia wakatumia nguvu yao ya fedha kuwachukua ndiyo maana tunataka kuendeleza mwendo wetu wa kimyakimya dirisha hili dogo,” alisema.

Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera, aliweka bayana kwamba, anataka kusajili wachezaji kadhaa katika nafasi ya beki wa kati, kiungo, winga, lakini pia straika, ili kuhakikisha msimu huu wanatwaa ubingwa.

Zahera alisema anayo majina mkononi mwake ya wachezaji watatu kutoka DR Congo, lakini pia taarifa nyingine zikidai kuwa Eliud Ambikile wa Mbeya City na Salum Kihimbwa wa Mtibwa Sugar, wameingia kwenye rada za wanajangwani hao.

MWENYEKITI

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.