Niyonzima mwili Simba, moyo Azam

Dimba - - News - NA SAADA SALIM

KIUNGO wa Simba, Haruna Niyonzima, amevunja ukimya na kudai kwamba akimaliza mkataba wake na Simba na kama hawatamuhitaji tena, ataangalia maisha mengine lakini hawezi kurudi Yanga.

Niyonzima, aliyesajiliwa Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Yanga msimu wa 2017, mkataba huo unamalizika mwishoni mwa msimu huu na amesema anaweza kusepa akiona mambo hayakai sawa.

Akizungumza na Dimba jana, kiungo huyo alisema mipango yake ni kuendelea kutumikia klabu yake ya Simba, lakini mkataba wake ukiisha na wenye timu yao wakashindwa kuonyesha nia ya kumuongezea mkataba, ataondoka.

“Unajua nimeishi kwa presha kubwa sana tangu nimekuja kucheza hizi timu kubwa, hivyo sijafikiria kurejea tena katika klabu yangu ya zamani (Yanga), kama sitaongeza mkataba Simba basi bora nikacheze timu nyingine.

“Sasa nimechoka maisha ya presha, hata nikirudi Yanga yatakuwa ni yale yale, bora kutafuta timu mbali na hizi, kucheza kwa amani pia inawezekana nikaachana na soka la Tanzania, hivyo yote yanawezekana,” alisema Niyonzima.

Taarifa nyingine zinadai kuwa, kiungo huyo huenda akatimkia Azam FC, kuwafuata marafiki zake Donald Ngoma pamoja na Obrey Chirwa, ambao walitengeneza kombinesheni kali walipokuwa wakiichezea Yanga.

Taarifa hizo zinadai kuwa, hata kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van de Pluijm, anamhusudu sana kiungo huyo na angependa kuungana naye kwa mara nyingine, kwani anaiheshimu kazi yake.

Katika hatua nyingine, Niyonzima amesema ana amani ndani ya kikosi cha Simba, tofauti na wengine wanavyodhani na sasa anajiandaa kurejesha makali yake kama ilivyokuwa mwanzo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.