Simba, vita dhidi ya Swallows si haba

Dimba - - News -

NOVEMBA 27 au 28, mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, wataanza safari kuelekea kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuivaa timu ya Mbabane Swallows ya Swaziland, katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote vile, Simba wataingia uwanjani wakitarajia kupata ushindi kabla ya mechi yake ya marudiano itakayochezwa Desemba 4 au 5 nchini Swaziland. Sisi Dimba ni miongoni mwa wadau wa soka hapa nchini tunaoamini kwamba, ushindi kwa Simba si mjadala tena, kwani klabu hiyo kwasasa ina kila sababu na nia ya kushinda. Aidha, tunafahamu kwamba mchezo huo utakaochezwa katika ardhi ya Tanzania, utakuwa ukifanyika mbele ya halaiki ya mashabiki wa mchezo wa soka, hiyo itawapa ari wachezaji kujituma ili kupata ushindi. Lakini kama ilivyokuwa dhana ya vita kukosa macho, timu ya Simba inatakiwa kuondoa matarajio ya kushinda nyumbani eti kwa vile tu itakuwa kwenye uwanja wake, tena mbele ya mashabiki wake, la hasha. Bali inachotakiwa ni kuihesabu mechi hiyo kama ni kibarua kigumu kwao kinachohitaji kupambana vilivyo ili kupata ushindi, vinginevyo lolote linawezekana. Ni kwa muktadha huo unaotufanya tuwakumbushe Simba, hasa benchi lao la ufundi kwamba, timu iliyopo mbele yao si ya mchezo mchezo na kama watataka kuhakikisha, basi majirani wao wa Azam FC wanaweza kuwa mashahidi wazuri. Ukiangalia takwimu chache tu za mafanikio ya klabu hiyo utaona jinsi ilivyoweza kukusanya mataji saba kati ya mwaka 1993 hadi 2018. Pia klabu hiyo imewahi kutwaa mataji ya FA mara nne, ukiachilia mbali mataji mengine ya michuano mbalimbali. Tunachotaka kusema, ni timu yetu kujipanga kila kona ndani na nje ili kuhakikisha hakuna mwanya wowote utakaosababisha timu hiyo ya Tanzania kukosa ushindi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.