Simba yajibu mapigo Yanga

Dimba - - Dimba - NA SAADA SALIM

WAKATI Simba wakicheza jana dhidi ya Mbabane Swallos mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kuibuka na ushindi wa mabao 4-0, baadhi ya viongozi wao wamelazimika kubakia jijini Dar es Salaam kuweka mambo sawa kutokana na kutishwa na kasi ya Yanga.

Yanga ndio ambao wanaongoza ligi wakiwa na pointi 38 katika michezo 14 waliyocheza lakini kinachowatisha sana Simba ni vipigo vikali wanavyovitoa wapinzani wao hao huko mikoani na hivyo kutishia ubingwa wao.

Vigogo hao wa Simba waliamua kuikacha safari ya kwenda nchini Eswatini zamani Swazland, kuishuhudia timu yao ikipepetana na Mbabane Swallows na kubakia jijini Dar es Salaam kwa kazi maalumu ya kuhakikisha klabu yao inategua mitego ya wapinzani wao na kujitengenezea mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao.

Ofisa Mwendeshaji wa Simba (C.O.O), Anorld Kashembe, amelithibitishia DIMBA Jumatano kwamba yeye na baadhi ya viongozi wengine hawakuambatana na timu huko, Eswatini na badala yake wanaendelea na mikakati mingine jijini Dar es Salaam.

“Hatuwezi kusafiri viongozi wote, wengine tumeamua kubakia Dar es Salaam kuhangaikia mambo mengine kwani kama unavyojua kuna michuano ya Ligi Kuu inaendelea hivyo lazima tuendelee na mikakati ya ushindi,” alisema.

Licha ya kwamba Yanga wanaonekana kuwa na moto wa hali ya juu wakitoa vipigo kwa kila timu inayowasogelea, lakini kigogo huyo wa Simba amesema lazima watetee ubingwa wao kutokana na ubora wa kikosi chao.

Katika msimamo wa ligi, Simba wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 27 wakicheza michezo 12, huku Yanga wakiwa kileleni na pointi zao 38 na Azam FC wakifuatia katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 33.

Kinachowatisha zaidi Simba ni kutokana na ushindi mfululizo wanaoupata Yanga zaidi katika michezo yao ya mikoani ambayo awali ilionekana kama Wanajangwani hao wangepata matokeo mabaya kutokana na aina ya kikosi walichonacho.

Yanga wametoa dozi ya maana mikoani katika michezo yao mitatu waliyocheza wakianza na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui mchezo uliochezwa Uwanja wa Kambarage, mkoani Shinyanga kabla ya kuibuka na ushindi kama huo dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba na Jumatatu iliyopita wakiwalaza Prisons mabao 3-1.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.