Mrithi wa Kapombe kuivaa Azam FC

Dimba - - Dimba - NA SAADA SALIM

UONGOZI wa Simba unapambana kuhakikisha wanapata hati ya uhamisho ya kimataifa (ITC) ya beki wao mpya, Zana Coulibally, ili awahi kucheza mechi yao ijayo dhidi ya Azam FC.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watacheza na Azam FC mchezo unaokuja ambao unatarajiwa kuchezwa Desemba 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na huenda Zana akacheza.

Coulibally aliyewahi kukipiga Asec Mimosa ya Ivory Coast, amekamilisha dili la kusajiliwa na Simba akiingia mkataba wa miaka miwili ambayo lengo kubwa la kusajiliwa kwake ni kuziba pengo la Shomari Kapombe anayepatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Ofisa Mwendeshaji wa Simba (C.O.O), Anorld Kashembe, alisema uongozi unahangaikia ITC ya beki huyo na muda wowote wanaweza wakaipata ili kujumuika na kikosi katika harakati za kutetea ubingwa wao.

“Tumeshawasiliana na Asec ili ndani ya wiki hii tupate ITC ya beki wetu huyu mpya, tunataka aanze kutumika hasa michezo yetu ya Ligi Kuu inayokuja mbele yetu, nadhani zoezi hilo litakamilika mapema,” alisema.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo, alifafanua kwamba mchezaji yeyote ambaye ITC yake itafika mapema na akapata leseni ya kucheza hatakuwa na kipingamizi.

“Mchezaji kutoka nje ya nchi ambaye amesajili na ITC imefika mapema, Shirikisho nao wakawahi kutoa leseni huyo moja kwa moja ataruhusiwa kucheza michezo ya Ligi Kuu, tunachokiangalia ni uhalali wa ITC yake,” alisema.

Ndimbo alitolea mfano wa straika wa Azam, Obrey Chirwa ambaye ITC yake imewasili juzi na hakucheza mechi ya jana dhidi ya Stand United kutokana na kuchelewa kupatikana kwa leseni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.