Kocha Zahera apata mrithi wa Yondani

Dimba - - Dimba - NA MWAMVITA MTANDA

KOCHA mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kama beki wake kinda, Cleofasi Sospeter, anaweza kuwa mbadala wa nahodha wa kikosi hicho, Kelvin Yondani.

Zahera alimpa nafasi kwa mara ya kwanza beki huyo katika mechi yao dhidi ya JKT Tanzania akiingia kipindi cha pili na kuonyesha uwezo mkubwa uliomvutia kocha huyo Mkongomani.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Zahera alisema beki huyo ana uwezo mkubwa sana na kama atajituma vilivyo bila shaka atarithi mikoba ya Yondani.

“Huyu mchezaji namuona kama dhahabu nyingine ndani ya kikosi cha Yanga, kwanza anayo mapenzi ya dhati na mpira kutokana na namna anavyocheza lakini pia hata mwili wake unamwonyesha kama mchezaji.

“Atafuata nyayo za Yondani (Kelvin) kama atajitunza na kuzidi kuupenda mpira, anaweza pia asiishie Tanzania na badala yake akachezea timu kubwa nje ya nchi,” alisema.

DIMBA Jumatano lilimtafuta beki huyo ili kujua anachukuliaje sifa kemkem anazomwagiwa na kocha wake, ambapo alisema atajitahidi kuzingatia mafundisho yake kwani anataka siku moja awe mchezaji mkubwa.

“Kwanza namshukuru kocha (Zahera) kwani yeye ndiye aliyeniona nikiwa kikosi B akanileta huku timu kubwa, niseme tu kwamba nitapambana sana kwani nahitaji kuwa mchezaji mkubwa," alisema.

JEMBE

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.