Solari hawezi kumtupa Miguelito Baeza

Dimba - - Dimba -

K AMA Javi Sanchez kapewa nafasi kikosi cha kwanza kwanini ishindikane kwa Miguelito Baeza? Kama Sergio Reguilon amepandishwa kikosi cha kwanza kutoka Castilla, kwanini ishindikane kwa Miguelito?

Kama Vinicius Junior mwenye miaka 18 anapewa nafasi na kutarajiwa kutamba iweje ishindikane kwa kocha Santiago Solari kumpa nafasi Baeza?

Uzuri. Javi, Vini, Reguilon wote wamepewa nafasi zaidi na kocha Santaigo Solari aliyekuwa akifundisha vijana Castilla. Miguelito mwenye miaka 18 alipandishwa kutoka kikosi cha chini ya 18 hadi ya 19.

Lakini kocha wake alikuwa Guti ambaye ameenda Besiktas.

Ninapowatazama vijana wa Real Madrid hakika napagawishwa mno na kujifunza namna nzuri ya uongozi si kwenye michezo tu hata maeneo mengine.

Ninaweza kutazama mechi za watoto chini ya miaka 10 Real Madrid. Nitahamia kwenye watoto chini ya miaka 15, kisha kuwatazama vijana wa chini ya miaka 19 na kumalizia vijana wa Castilla.

Kila kundi lina vijana wanaonivutia mno katika soka. Jinsi wenzetu wanavyohusudu soka. Jinsi wazazi wanavyohangaika kuhakikisha wanalipia mafunzo ya watoto wao ili kutimiza ndoto zao.

Jinsi watoto wenyewe wanavyohangaika kujiweka kwenye hali ya kuwa vipaji bora. Kwenye kikosi cha Castilla nilivutiwa na uwezo wa Sergio Diaz, Javi Sanchez na Febas ambaye kwa sasa yuko Real Zaragoza kwa mkopo.

Ninatazama mechi za watoto wa Real Madrid kwa kila umri na timu za wakubwa. Kama kuna daktari ambaye angeniona mechi ninazotazama basi angesema naumwa.

Lakini mwisho wa siku ningekuwa nawashangaa tu kwa sababu hicho ndicho kilevi changu nambari mbili; mpira baada ya namba moja; vitabu na kuogelea.

Kati ya wote hawa namkubali zaidi Miguel Baeza. Ukimwangalia uchezaji wake utaona ni kiungo mmoja mtamu mno. Lakini Baeza pia kiungo mshambuliaji na winga kama ilivyokuwa kwa Guti mwenyewe.

Jina lake la utani ni Miguelito. Guu lake la kushoto hunikumbusha uhondo wa Guti au Santiago Solari mwenyewe walipokuwa wachezaji.

Katika umri wake Miguelito amekuwa akichanganya staili.

Unaweza kumfananisha na Steve McManaman, yule mwingereza aliyezaliwa kuichezea Real Madrid peke yake maana kule Liverpool alipotea tu.

Baeza ni mmoja wa kipaji ambacho huwa kinanisisimua na kuona kuwa Real Madrid ina watu wa mpira. Watu wanaojua kukisoma kipaji na kukabidhi kwenye njia sahihi.

Miguelito ni hatari sana kwenye winga. Ni hatari kwenye kiungo. Ni hatari mwenye mashuti. Ni hatari kwenye kasi. Miguelito ni mkali pia kwenye mashambulizi ya kushtukiza. Ana mguu mwepesi wa kushoto na udambwidambwi wa kutosha.

Anaweza kupiga mapande ya nguvu. Na zaidi ana ile tabia ya mabao ya visu kama Toni Kroos. Kwamba hawatumii nguvu nyingi lakini jinsi wanavyoukata mpira na unavyotinga wavuni unabaki mdomo wazi, wamewezaje.

Miguelito ni zao fulani kama Isco, Solari mwenyewe, Clarence Seerdof, au kama unamkumbuka Khalilou Fadiga wa Senegal au Bradley Carnel yule mchambuzi wa soka wa Supersport, enzi zake akikontroo mpira kwenye guu la kushoto, utainuka kushangilia.

Uchezaji wa Miguelito Baeza unavutia mno. Ndio maana sitashangaa kuona kocha wetu Santiago Solari akimfanya Miguelito kuwa sehemu ya jeshi lake jipya analojaribu kulijenga Real Madrid.

Yaani jeshi la kizazi kipya cha soka klabuni baada ya miaka ya kutamba nakufyekelea mbali wote.

Baeza kwa sasa amechezea timu ya taifa ya Hispania chini ya miaka 16, 17 na sasa 19. Miguu yake inapokokota mpira hunikumbusha madoido ya McManaman aua Luis Figo.

Miguelito ni toleo jipya la Real Madrid. Kama kuna siku nikiulizwa kuchagua wawili kati ya James Rodriguez (yupo kwa mkopo huko Bayern Munich) na Miguelito nani awe kwenye kikosi chetu kwa sasa nitakutajia huyu dogo Baeza.

Kwanza ana miaka 18. Anahitaji mwaka mmoja kupewa dakika na msimu wa pili kuwachachafya wapinzani. Kwa hatua ya sasa ya kumwita mazoezini ni moja ya bingo.

Ni kamari bomba sana kwakuwa kipaji chake si cha kusema asubiri kwanza bali aendelezwe zaidi. Ukitaka mabao ya faulo, mpe mpira Miguelito.

Ukitaka chenga ndani ya boksi la adui, mpe pasi Miguelito. Ukitaka kuwalaza na viatu mabeki wa timu pinzani, mpe pasi Miguelito.

Ukitaka kuona burudani ya mpira miguuni basi subiri Miguelito apewe mpira halafu aanze tu mbio zake za KiMcManaman, Raul, Guti, Asensio au Zidane.

Baeza alijiunga na Real Madrid akiwa na miaka 6 tu. Hadi leo anaendeleza cheche zake. Unapokuwa na mchezaji ambaye anaweza kuwalamba vyenga mabeki wanne hadi watano ujue ni bingo.

Ni kama bomu la nyukilia aiseee! Miye nahusudu kutazama Miguelito, anapokokota mpira na kufunga mabao, ni udambwidambwi mtupu. Narudia, simiani kama Santiago Solari anaweza kumaliza msimu huu bila kumwita kijana mazoezini ama kumwandaa kwa ajili ya mechi yoyote hata za kombe la mfalme.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.