Kiilichomliza Zahera Mbeya hiki hapa

Dimba - - Dimba - NA HUSSEIN OMAR,MBEYA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kilichomfanya amwage machozi baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Tanza- nia Prisons, ni kutokana na timu yake kupata matokeo katika mazingira magumu.

Kikosi hicho cha Yanga kiliendeleza ubabe wake mikoani kikiwafunga Prisons mabao 3-1 mchezo uliochezwa Jumatatu ya wiki hii Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Zahera alisema alijikuta akimwaga machozi akiwaza namna mwamuzi wa mchezo huo, Meshack Sudi, alivyoionea timu yake lakini mwisho wa dakika 90 wakaibuka na ushindi.

“Unajua yule mwamuzi alifanya maamuzi ya kutuonea sana, mimi naliomba Shirikisho la Soka nchini (TFF), wamwangalie vizuri kwani anaweza akasababisha matatizo makubwa,” alisema.

Mbali na hilo, Zahera anasema wachezaji wake wanapitia mazingira magumu ya kukosa mishahara lakini wamekuwa wakijituma na kupata matokeo mazuri tofauti na wengi walivyokuwa wakiwachukulia.

Yanga wamecheza michezo 14 wakishinda michezo 12, sare michezo miwili wakiwa hawajapoteza mchezo wowote wakiwa kileleni na pointi zao 38 huku wakishinda michezo yao yote mitatu ya mikoani.

Walianza kuwafunga Mwadui FC mabao 2-1 mchezo uliochezwa Uwanja wa Kambarage, mkoani Shinyanga kabla ya kuibuka na ushindi kama huo dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba na Jumatatu iliyopita wakiwalaza Prisons mabao 3-1.

Katika hatua nyingine, wanachama na mashabiki wa Yanga wanaoishi Tunduma, mkoani Mbeya, jana walilisimamisha basi la timu hiyo na kumbeba juujuu kocha Zahera kutokana na kuridhishwa na kazi anayoifanya.

KISASI

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.