Vigogo TFF wamkimbia Wambura

Dimba - - Dimba -

NA CLARA ALPHONCE MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, aliyetoka kifungoni jana, alitinga kwa kishindo katika ofisi za Shirikisho huku vigogo wenzake wakimkwepa.

Wambura alifika katika ofisi hizo zilizopo Ilala, Karume saa 11.30 akiongozana na Wakili wake, Emmanuel Muga na moja kwa moja waliingia ndani na kupokewa na baadhi ya wafanyakazi wa TFF, huku viongozi wa juu wote wakiwa wameingia mitini.

Safari ya Wambura ofisi za TFF ilikuwa ni kwenda kukabidhi barua ya hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, iliyotengua maamuzi ya Kamati za Maadili za shirikisho hilo kumfungia maisha kujihusisha na masuala ya soka.

Tukio la Makamu huyo wa Rais kwenda ofisini kwake kwa mara ya kwanza lilivuta hisia za watu wengi, vikiwemo vyombo vya habari ambavyo vilipiga kambi tangu asubuhi na mapema.

Moja ya picha kubwa iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ni namna ambavyo Wambura angepokelewa na hasimu wake, Rais Wallace Karia na Katibu Mkuu, Wilfred Kidau, ambao hawakuwapo ofisini.

Ilipofika Saa 11.45 Wambura na wakili wake walitoka nje ofisi hizo na kuzungumza na Waandishi wa habari ambapo alisema, amekuja kutekeleza majukumu aliyopewa na Mahakama Kuu kwa kuwasilisha hukumu kabla ya kukalia kiti chake.

"Sijakuta maofisa wengi ofisini zaidi ya Mkurugenzi wa Fedha na wahudumu wengine wa chini, ila kikubwa nimeweza kutimiza masharti ya Mahakama ambayo kwanza ni kuripoti ofisini, pili naleta taarifa ya mahakama ambayo imepokelewa na nimeweza kufika, kama utekelezaji hautafanyika basi nitarejea mahakamani.

ìLakini nashukuru kwamba kila kitu kimeenda vizuri na barua yangu imepokelewa na mmoja wa wahudumu wa TFF, ambaye ndiye nimeambiwa amepokea barua, kwa jina anaitwa Latifa,î alisema Wambura.

Machi mwaka huu Kamati ya Maadili ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Hamidu Mbwezeleni ilimfungia maisha Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa kumtia hatiani kwa makosa matatu ambayo ni kupokea fedha za TFF, malipo yasiyo halali na kughushi barua.

Kosa jingine ni kushusha hadhi ya TFF, jambo lililomfanya Wambura kufungua kesi mahakamani akipinga adhabu hizo.

Novemba 30 mwaka huu Mahakama Kuu ya Dar es Salaam kupitia kwa Jaji Benhajji Masoud ilitengua maamuzi ya Kamati hiyo ya Maadili ya TFF na kuamua kumrejesha Wambura kwenye nafasi yake.

Bosi huyo aliongeza kuwa Maamuzi hayo ya Mahakama, amepanga kuyapeleka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ili kutoa fursa kwa wengine ambao wamekuwa wakionewa na baadhi ya watu kukiuka kanuni.

ìKatika historia ya soka hapa nchini haijawahi kutokea ndani ya miezi sita tangu viongozi wapya kuingia madarakani na kufungia wajumbe watatu wa kamati ya utendaji,î alisema Wambura.

Mbali na kwenda Fifa, Wambura alisema ana mpango wa kukutana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe kwa ajili ya kuzungumza naye na kuona wapi anasaidia kuokoa soka la Tanzania.

UONGOZI

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.