Ilichofanya Simba, inastahili pongezi

Dimba - - Dimba -

TIMU ya Simba ya Tanzania, jana iliweza kukonga nyoyo za mashabiki wao, kufuatia ushindi mnono walioupata wa mabo 4-0 dhidi ya Mbabane Swallows, katika mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Mavuso katika jiji la Mazini, nchini Eswatini zamani Swaziland.

Ushindi huo umedhihirisha uwezo mkubwa wa kikosi cha Simba, ambacho awali kilipata matokeo ya ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.

Sisi Dimba tunaungana na wapenda kandanda wote nchini waliofurahia ushindi huo, tunaamini ni mwanzo mzuri kuelekea hatua ya pili ya michuano hiyo.

Hatuna wasiwasi kwamba, baada ya vipigo hivyo vivili vya nguvu, Simba itafanya tena mauaji kama hayo pale itakapowavaa Wazambia Nkana Red Delvis, timu ambayo ndiyo itakayokutana nayo katika hatua inayofuata.

Tunaupongeza ushindi kwa maana kubwa kwamba, licha ya kikosi hicho kuweza kusonga mbele, lakini itakuwa ni hatua nzuri ya kutekeleza agizo la Rais wa Tanzania, John Magufuli, kuitaka timu hiyo ijipange kupata ushindi katika michuano ya kimataifa.

Kana kwamba haitoshi, Simba, wachezaji wa timu hiyo watakuwa wamejibu kwa vitendo agizo la Mdhamini wao Mkuu, Mohamed Dewji, aliyeagiza ushindi wa mechi hizo mbili kama hatua yake ya kwanza kuelekea maandalizi ya Simba anayohitaji kuiona.

Dewji alionekana kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Taifa, Jumatano ya Novemba 28, akiishuhudia timu yake hiyo ikitoa kipigo kwa Waswazi hao.

Tunarudia kuipongeza Simba, lakini tukitoa tahadhari pia kwamba ushindi huo mkubwa usiwafanye wachezaji hata viongozi wa benchi la ufundi pamoja na wadau wengine kubweteka.

Kwani bila kujiandaa vya kutosha, timu inaweza kupotea malengo na kujikuta wakiishia njiani ilhali mikakati ya sasa ni kusonga mbele. Hongereni Simba na kila la heri katika maandalizi ya mechi ijayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.