Najivunia kumjengea nyumba mama yangu

Dimba - - Dimba -

NA CLARA ALPHONCE M WAKA 2015 usajili wake kutoka Kimondo FC ya Mbeya kwenda Yanga, ulizusha mvutano mkubwa wa kisheria kabla ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuingilia kati na kuweka mambo sawa.

Hapo ndipo nyota ya Godfrey Mwashiuya ilipoanzia kung'ara akiwa ndani ya Yanga na kujikuta akifanikiwa kupenya hadi kikosi cha kwanza chini ya kocha, Hans Pluijm.

Winga huyo wa kushoto kwa sasa ni mchezaji huru akitokea Singida United ambako ametimka baada ya mkataba wake na klabu hiyo kuvunjika kutokana na kukiukwa kwa baadhi ya vipengele.

DIMBA limemtafuta Mwashiuya na kupiga naye stori mbili tatu kuhusiana na maisha yake nje ya soka na haya ndiyo majibu yake.

DIMBA: Nje ya soka wewe ni mtu wa aina gani? MWASHIUYA: Ni mtu wa

watu nacheka na kila mtu, bila kujali mkubwa au mdogo. DIMBA: Unaishi wapi na nani?

MWASHIUYA: Mtoni Kijichi, jijini Dar es Salaam na familia yangu mke na mtoto mmoja anaitwa Barba.

DIMBA: Kama Mungu akikujaalia umepanga kuzaa watoto wangapi na jinsia gani?

MWASHIUYA: Watoto watatu jinsia wa kiume wawili na wa kike mmoja, ila ikitokea nikapata wa kike nitashukuru tu kwa kuwa siwezi kumpangia Mungu mipango yake. DIMBA: Kuna siku umeshawahi kutamani kuoa wake wawili? MWASHIUYA: Hapana, sijawahi kwanza dini yetu hairuhusu kuoa wake wawili. DIMBA: Unapenda kula chakula gani? MWASHIUYA: Napenda sana pilau kwani ni moja ya chakula ambacho nakipenda na hata mke wangu analijua hilo.

DIMBA: Siku ambayo unaenda kucheza mechi huwa unakula

chakula gani? MWASHIUYA: Mara nyingi nakula matunda tu ili niwe mwepesi. DIMBA: Mara ngapi kwa mwezi unavaa shati na suruali ya kitambaa? MWASHIUYA: Kwa mwezi navaa mara tatu hasa nikiwa naenda Kanisani. DIMBA: Unapenda kuvaa mavazi gani sana?

MWASHIUYA: Napenda kuvaa sana suruali. Vazi la pensi silipendi kwani mimi ni mtu mzima hivyo kuacha baadhi ya viungo vyangu wazi si jambo lenye afya.

DIMBA: Kwa mwezi unatenga kiasi gani kwa ajili ya mavazi?

MWASHIUYA: Huwa sina utaratibu sana wa kutenga fedha kwa ajili ya mavazi ila kwa mwezi naweza kununua nguo mbili, kwa sababu mimi si mpenzi sana wa vitu hivyo. DIMBA: Ili uonekane mtanashati hasa katika upande wa nywele, huwa unatumia kiasi gani saluni? MWASHIUYA: Kama Sh 15,000 tu. DIMBA: Unapenda kuendesha gari ya aina gani? MWASHIUYA: IST. DIMBA: Ikitokea dili ya mavazi, wewe ungependa kuvalishwa na kampuni gani? MWASHIUYA: Nike. DIMBA: Unapenda marafiki wa aina gani? MWASHIUYA: Hasa wanaojielewa na kujitambua, wapenda maendeleo. DIMBA: Chakula chako cha kwanza kupika kilikuwa nini na ilikuwaje siku hiyo? MWASHIUYA: Ilikuwa chai, nilipika vizuri kwa sababu mke wangu alikuwa karibu kunielekeza. DIMBA: Unatarajia kuwa na maisha gani baada ya soka? MWASHIUYA: Mfugaji na mkulima. DIMBA: Starehe yako kubwa ni nini? MWASHIUYA: Kusikiliza nyimbo za asili.

DIMBA: Mkeo ana nafasi gani katika ushauri wa masuala ya maisha? MWASHIUYA: Yeye ndio mtu wa karibu yangu namba moja ambaye napanga naye mipango yetu ya kila siku.

DIMBA: Fedha yako ya kwanza ya usajili ulifanyia kitu gani?

MWASHIUYA: Najivunia nilifanya kitu cha maana kwa kumjengea nyumba mama yangu mzazi huko kwetu Mbozi.

DIMBA: Msanii gani wa Bongo Fleva unapenda kusikiliza kazi zake? MWASHIUYA: Best Naso. DIMBA: Mke wako anapenda umfanyie kitu gani ambacho kinamfurahisha? MWASHIUYA: Nikimnunulia nguo au vitu vingine anafurahi sana. DIMBA: Kitu gani ukimfanyia anakasirika sana. MWASHIUYA: Kurudi nyumbani usiku, nikifanya hivyo anaona kama simpendi basi siku hiyo hatuelewani kabisa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.