Hurrem sultana, ibrahim pasha watifuana

Dimba - - Dimba - NA BRIDGETTE EMMANUEL

K ARIBUNI wasomaji wa gazeti la DIMBA, hususan wale mnaofuatilia tamthilia ya Sultan inayorushwa kila siku kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa kupitia chaneli ya Azam Two. Toleo lililopita tuliona jinsi Sultan alivyoanza kumtilia shaka Ibrahim Pasha kuwa huenda anamzunguka na zaidi ya hapo Hurrem anamfanyia fitna kupitia kwa Rustem kiasi kwamba Ibrahim anajikuta akikataliwa na watu kila kona kiasi kwamba baadhi wanafikia mbali na kumtaka aachie ngazi, ni nini kinafuata? Endelea kuisoma...

Ibrahim, huku akiwa amevurugwa na makelele ya watu wanaomzomea na kumponda kwamba yeye si Muislamu safi na ndiyo maana alikataa kuchukua hata kitabu kitukufu cha Koran alichopewa zawadi, huku pia akidaiwa kutengeneza masanamu na kuabudu dini ya Kikristo kisirisiri, anakasirika sana.

Anaamua kumvaa mmoja wa watu waliomshambulia kwa maneno, lakini kwa bahati nzuri askari wanamzuia, lakini anaagiza mtu huyo aende kutupwa jela mara moja na ikiwezekana anyongwe.

Upande mwingine, Suleiman, akiwa peke yake sebuleni kwake anakumbuka jibu alilowahi kujibiwa na Ibrahim kwamba iwapo ataambiwa achague kifo cha aina gani, atapendelea afe kifo kama cha Sultani wake ambaye ni rafiki, kaka na mshauri wake mkuu na kwamba hapo ndipo roho yake itakuwa na amani.

Kisha Hurrem anakuja na kumuuliza kinachomfanya Sultan awe na mawazo mengi kiasi kile, naye anajibu kuwa yule binti aliyejiua (Gulizar) alitaka kumuua mwanawe Mustafa, lakini minong'ono iliyoko mitaani ni kwamba yeye Hurrem ndiye aliyemtuma kufanya hivyo.

Hurrem anamjibu kuwa huo ni uwongo wa Ibrahim. Kisha Suleiman anamuuliza Hurrem ni lini ugomvi kati yake na Ibrahim utakwisha, lakini anajibiwa Ibrahim ndiye mwenye makosa.

Baadaye Suleiman anamuuliza tena Hurrem ni nini kilichojaa ndani ya moyo wake na yeye anajibu kuwa ni mapenzi mazito tu juu yake Sultan.

Kule Manisa Fatma anamwambia Mustafa kulipa kisasi juu ya kifo cha mwanawe ili kumpa Hurrem maumivu sawa na wao waliyoyapata, huku akidai anadhani kuwa ndiye aliyesababisha mtoto wao huyo akafariki.

Mustafa anabaki kimya tu akimtazama bila kusema chochote.

Upande mwingine kule sokoni jijini Istanbul, mtu mmoja aliyetumwa na Rustem anaonekana kuwajaza watu upepo kwa kutoa tuhuma mbalimbali dhidi ya Ibrahim Pasha.

Mtu huyo anawakumbusha watu kuhusu Ibrahim jinsi anavyotaka kumnyonga mtu asiye na hatia. Watu wanajawa na hasira na kuamua kwenda kwa Ibrahim kwa ajili ya kudai haki na kutaka mtu yule aachiwe huru.

Naye Ayaz Pasha anakwenda kuchongea kwa Sultan kuhusiana na zogo lililotokea kule sokoni na kwamba Ibrahim Pasha alifanya maamuzi ya kutaka mtu anyongwe bila ya kesi yake kusikilizwa.

Huku nako Sah Sultan anashangaa baada ya kusikia kuwa mpaka wakati huo, Ibrahim Pasha hana habari kuhusu ujio wake. Wanazungumza mawili matatu baada ya kusalimiana, lakini kelele za watu zinaanza kusikika nje ya nyumba yake.

Na Ibrahim anaposikia kelele zikizidi nje ya nyumba yake, kwa hasira anakwenda kuwatishia watu kwamba kama hawataondoka atawahukumu kunyongwa.

Sah Sultan anashangaa kwa nini watu wanaonekana kutoridhishwa na Ibrahim, lakini Hadija Sultani anamwambia kwamba ni vigumu kuwaridhisha watu wote kwa pamoja lazima patokee watu wa kupinga tu.

Hadija Sultan anamwambia kwamba ni lazima afikirie kitu kwani Hurrem anataka kuwaua Ibrahim na Mustafa na kwamba hatma ya urithi wao wa Ufalme, iko mashakani.

Kauli hii inamfanya Sah kushangaa iwapo Hadija Sultan anafikiria kuhusu suala la urithi wa kiti cha Ufalme au mumewe, Ibrahim Pasha.

Upande mwingine Sultan anamuuliza Ibrahim kwamba inawezekanaje anaamua kumuweka mtu gerezani bila kufuata sheria, tena katika kipindi hicho cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani na zaidi ya hapo anataka anyongwe kabisa?

Suleiman pia anasema kwamba hatamnyonga mtu yeyote bila hukumu yake kuamriwa na Jaji na amri nyingine za akina Ayaz Pasha, jambo linalomkosesha amani Ibrahim.

Huko Manisa nako anaonekana Mustafa akilia mwenyewe kimya kimya. Anayakumbuka maneno ya baba yake aliyowahi kumwambia kwamba mwanamume anaweza kulizwa na vitu viwili tu, mapenzi na kifo.

Naye Mahidevran anaamini kwamba kifo cha mwanawe hakikuwa cha bahati mbaya, kimetengenezwa na anampa Diana majukumu ya kufanya.

Kwenye bustani kule mjengoni Hurrem anampa zawadi Rustem kwa kufanikisha dili la kumchafua Ibrahim na kumtaka awe anampa taarifa zote.

Ndani ya mahakama Ayaz Pasha anamtaarifu Jaji kila kitu kilichotokea kuhusu Ibrahim, huku Ibrahim naye akimwelezea Matrakci jinsi alivyosikitishwa na maamuzi ya Sultan, akidai kuwa yote haya yanasababishwa na mtego aliotegewa na Hurrem ili Sultan asiwe na imani naye. Matrakci anamjibu kuwa maamuzi ya Sultan ni ya haki.

Huku nako Sultan anaonekana akimuaga Rustem, aliyepewa cheo cha kwenda kuongoza jimbo jingine na baada ya kuagana Rustem anapokutana na Mihrima anamwambia kwamba ana bahati kubwa kukutana naye kabla ya kuondoka. Naye Nigar ambaye ni mke wa Rustem anakwenda kumuaga binti yao anayelelewa nyumbani kwa Ibrahim Pasha.

Kwenye mlo wa futari Hurrem anagundua kuwa Hadija Sultan hali wala hanywi kitu chochote na wala hazungumzi na mtu yeyote na anagundua kuwa ameghadhabishwa na kile kilichotokea kwa mumewe anayetuhumiwa vibaya na umati wa watu.

Hurrem anasema kwamba uamuzi huo wa watu si wa siku zote, ni suala la muda tu, jambo linalomvuruga Hadija Sultan ambaye anataka kuwaka, lakini anatulizwa na Sah. Hadija Sultan anaamua kuondoka na kuwaacha Sah na Hurem.

Gulfem anaamua kumfuata na Hadija anamueleza kuwa haoni kama Sah Sultan atamsaidia kumuondoa Hurrem katika familia yao na anaona kama hakutoa wazo zuri kumuita aje kwao katika kipindi hicho cha mwezi wa Ramadhani.

Naye Hurrem, huku wakiwa wamekaa wawili tu na Sah, anatumia muda huo kumwambia umbeya kuhusu mahusiano ya Ibrahim na Nigar na kuhusu mtoto ambaye kila mmoja alijua kuwa amefariki na kwamba Hadija alimsamehe Ibrahim.

Muda huo huo Nigar anamwambia Ibrahim amtunze vizuri mtoto wao na asimsahau yeye kama mama wa mtoto, huku akisisitiza kuwa moyo wake bado uko juu yake.

Hadija Sultan naye anakwenda kulalamika kwa Sultan kwa kuingilia kesi ya Ibrahim, huku akisema kwamba ni Ibrahim huyo huyo amekuwa akiokoa taji la urithi kwa miaka mingi, lakini Sultan anamjibu kwamba ni wajibu wa Ibrahim kufuata sheria na haki.

Huku nako nesi anayemhudumia Nurbahar (Clara) anamwambia asimweleze mtu yeyote kama ametoa mimba.

Naye Mihrimah anamkatalia katakata Mehmet kwamba kuna kitu kinaendelea kati yake na Yahya na anapouliza ni kwa nini alimtishia Clara, anasema sababu ilikuwa ni kutopoteza uaminifu wake kwa baba yao.

Mehmet anauliza iwapo kuna suluhiso jingine la mimba ya Clara zaidi ya kuitoa lakini Mihrimah anamjibu tofauti.

Nako Manisa, Fiden anamwambia Mahidevran, kwamba Ayse ni mjamzito, jambo linalomfurahisha sana Mahidevran ambaye anakwenda kumwambia Mustafa.

Mahakamani nako kesi ya mfanyabiashara na Ibrahim inaanza kusikilizwa na Jaji anamuuliza mfanyabiashara yule kama aliwahi kumuona Ibrahim akiabudu masanamu na anajibiwa kwamba kamwe hajawahi kuona kitu kama hicho, isipokuwa watu wote kule sokoni wanazungumzia suala hilo.

Katika maswali mengine mfanyabiashara anajikuta akijibu kuwa ni kweli kwamba amekuwa akimuona mfanyabiashara yule akisali msikitini mara kwa mara.

Baada ya mahojiano ya muda, Jaji anaamuru mfanyabiashara yule aadhibiwe na kisha atengwe kwa kupelekwa sehemu iitwayo Rodes. Ibrahim anaridhika baada ya kuambiwa na Matrakci jinsi hukumu iliyokuwa.

Naye Sah anagundua kuwa Hadija Sultan amesononeshwa mno kuhusiana na kesi ya Ibrahim na anamwambia kwamba atahukumiwa kulingana na haki yake.

Pia anamwambia kwamba anajua kila kitu kilichotokea kati yake na Nigar, lakini Hadija Sultan anamjibu kuwa hiyo yote ni sababu ya Hurrem, ingawa Sah anamjibu kuwa anavyoona hakuna wa kulaumiwa.

Upande mwingine Sultan anamshukuru Jaji kwa kutoa hukumu ya haki na pia jaji anamtaarifu kuwa hakuna nyama ya kutosha sokoni na kujibiwa kuwa hilo litashughulikiwa.

Kwingineko Hurrem anapandwa na hasira anapoambiwa na Sumbul kuhusu kutopatikana na hatia kwa Ibrahim Pasha. Ibrahim naye anamuita Balozi wa Ufaransa ili ahudhurie hukumu na kushuhudia haki inavyotendeka ndani ya himaya ya Ottoman.

Rustem akiwa anashuhudia, ananong'ona kwamba mwisho wa Ibrahim unakaribia kabisa. Hurrem anamwomba Ayaz Pasa atafute jambo la kumchafua Ibrahim.

Huko Manisa Fiden anawaomba watu wa karibu kumlinda Ayse ambaye ana ujauzito wa Mustafa, huku akisema kwamba mtoto atakayezaliwa lazima atunzwe, kwani anaweza kuwa mrithi wa kiti cha ufalme kwa siku za usoni.

Ibrahim anakutana na Hurrem na kumzodoa kwamba mipango yake ya kumng'oa imekwama, hivyo hata akijifanya kuchangisha mifuko ya kusaidia jamii, hiyo haitamfanya aonekane mtakatifu.

Hurrem anamwambia asijishaue, kwani karibu ataondoka mjengoni na akiondoka hatarudi tena, ingawa hajui ataondoka kwa usafiri ama kwa miguu. Mehmet naye anamwambia Mihrimah aachane na mpango wa kumtoa mimba Clara, lakini Mihrimah anamjibu kwamba tayari amekwishachelewa.

Naye nesi anawambia Clara kuwa suala la mimba litakwisha karibuni, huku Kiraz akiwasikiliza. Mihrimah anamuona kwenye korido na kumwambia asimwambie yeyote kuhusu jambo hili.

Sultan naye anajiandaa kwenda msikitini lakini ghafla Ibrahim anakuja na kumuuliza iwapo amesikitishwa na hukumu ilivyotolewa na Ibrahim anamjibu hapana.

Ayaz Pasha anamwomba Sultan kusoma majadiliano ya kesi ya Ibrahim kwa Balozi wa Ufaransa na Sultan anabaki mdomo wazi kutokana na kile Ibrahim Pasha alichokisema, wakati Sultan alikuwa Manisa.

Fatma naye anaweweseka na anamtuhumu Ayse kwamba ndiye aliyemuua mwanawe. Mahidevran anamwambia Mustafa wamtimue Fatma kutoka pale mjengoni kwa sababu amechanganyikiwa na Fatma anapoligundua hilo, anaamua kunywa sumu na kufariki.

Huku kwingine Hurrem anajadiliana na Ayaz Pasha akisoma waraka alioletewa, huku akisema tangu Ibrahim aanze kujitapa kwamba yeye ni tai na yeye (Hurrem) ni njiwa atachunga sana jinsi ya kuzipeperusha habari hizo.

Ibrahim naye anamshukuru Jaji kutokana na uamuzi wa kesi yake na kushangaa imekuwaje amemuokoa wakati alikuwa na uwezo wa kumkandamiza lakini Jaji anasema kwamba ameamua kulingana na haki.

Ibrahim anashangaa iwapo Jaji huyo anaweza kuamua kwa haki kama kesi itamhusu mwanaye wa kumzaa, huku akimkumbusha kuwa hakuna mtu anayeweza kumdhuru (Ibrahim). Jaji baadaye anasema kwamba anaweza kujidhuru yeye mwenyewe.

Suleiman anasoma waraka wa Ibrahim jinsi alivyokutana na Balozi wa Ufaransa na kusema kwamba, ambapo Ibrahim aliwahi kusema kuwa kazi ya mfugaji wa wanyama wa mwituni ni kumfuga simba, jambo linalomfanya Sultan atabasamu.

Ghafla tabasamu la Sultan linayeyuka mdomoni anaposoma kwamba Sultan wa himaya ya Ottoman ndiye simba, na Ibrahim ndiye mfugaji wake, jambo linalomfanya anyamaze kimya na kutafakari.

Wakati Sultan akiendelea kutafakari kile alichokisoma, ghafla Ibrahim anaingia mle ndani. Anamtazama kwa tabasamu la hasira huku Ibrahim akiwa na shauku ya kutaka kujua kile kinachosomwa. Anamuuliza Sultan kama yuko sawasawa, kisha anamualika kwa ajili ya chakula cha usiku na wakati Ibrahim anapoondoka, midomo ya Suleiman inaganda, akijaribu kutafakari kile anachokisoma. Anajisikia uchungu kiasi fulani.

Mihrimah naye anamuona Kiraz akizungumza na Afife, anamtaka amtimue mle mjengoni na Afife anamtaafiru Hurrem. Mihrimah anamdanganya mama yake, kwamba Kiraz aligundua kukutana kwao na mshairi hivyo ameamua kumtimua.

Hurrem anaposikia hivyo anamuagiza Afife kumpeleka Kiraz huko Trabzon na asirudi tena. Afife anashangaa na kusisitiza ni bora wangemsikiliza na Kiraz ili kujua kilichotokea, lakini wanaambiwa hajui lolote.

Huku nako Yahya anamtaarifu Mustafa kuhusu taarifa za kifo cha Gulizar ambaye aliamua kujirusha ghorofani na kwamba alikataa kukiri kosa lake kwamba alitumwa na Hurrem.

Upande mwingine Suleiman yuko chumbani kwake anarudia kusoma maneno ya Ibrahim, haamini kile anachokisoma na ghafla Hurrem anaingia lakini Suleiman anamwambia amuache peke yake.

Akiwa kibarazani, anaitazama barafu inavyoanguka huku akitafakari kile alichokisoma huku akifikiria nini cha kumfanya Ibrahim.

Ibrahim anaandaa chakula cha usiku kwa viongozi wenzake na wakati Balozi wa Ufaransa anapokuja na kumpa zawadi ya kitabu cha Machiavelli, Ibrahim anasema kwamba kila mmoja ni lazima aogope kwa sababu kitabu kile kimeandikwa na shetani mwenyewe, hivyo hawezi kukipokea.

Sultan anakumbuka mwaka 1523, wakati alipomteua Ibrahim kuwa Waziri Mkuu na kukumbuka ahadi ya Ibrahim ya kumlinda.

Kwingineko Jaji anashtushwa na ujio wa ghafla wa Sultan. Sultan anaomba ushauri kwa adhabu aliyoitoa kwa yule mfanyabiashara, anaambiwa kwamba anastahili adhabu ya kifo, lakini akaomba alindwe asiuawe katika muda wote ambao Sultan atakuwa hai. Jaji anamuuliza Sultan ni kwa nini amefanya maamuzi hayo, naye anajibiwa kwa sauti. KUNYONGWA! Ni kwa nini ametamka neno hilo? Usikose kufuatilia mwendelezo wa tamthilia hii katika toleo la DIMBA Jumatano ijayo. Kwa maoni, ushauri 0718483268.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.