Rekodi zinaongea, Emery kuvunja mwiko kwa Mourinho leo?

Dimba - - Dimba - MANCHESTER, England

L IGI Kuu ya England itaendelea tena leo baada ya kutimua vumbi jana na mwishoni mwa wiki iliyopita kwa timu mbalimbali kushuka viwanjani kusaka pointi tatu.

Ilikuwa wikiendi ya michezo mikubwa ndani ya ligi hiyo maarufu duniani, Arsenal waligawa dozi nzito ya mabao 4-2 kwa Tottenham ndani ya Uwanja wa Emirates huku Liverpool akifunga pazia kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Everton.

Pamoja na klabu hizo kupata ushindi bado Manchester City wameendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu England na kupigiwa upatu wa kutwaa taji hilo kwa mara nyingine baada ya kufanya hivyo msimu uliopita.

Katika michezo ya Ligi Kuu England ambayo inatarajiwa kupigwa leo na kesho, Manchester United watawakaribisha Arsenal katika Uwanja wa Old Trafford baada ya kutoa sare ya mabao 2-2 na Southampton ndani ya Uwanja wa St. Mary.

Ni mchezo mwingine mkubwa kwa timu zote mbili, Arsenal ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 30 huku wenyeji wa mechi hiyo Manchester United wakisalia nafasi ya saba na pointi 22.

Kasi ya Arsenal chini ya Unai Emery imezidi kuwa kubwa baada ya kushinda michezo zaidi ya 15 katika michuano yote waliyoshiriki msimu huu huku vijana wa Jose Mourinho wakionekana kusuasua kwa kutokuwa na mwendelezo mzuri wa ushindi.

Lakini pamoja hayo, kocha wa Arsenal, Emery hana rekodi nzuri anapokutana na Mourinho ikiwa wamekutana kwenye michezo mitano ambayo iliisha kwa Mreno huyo kushinda mara nne na sare moja. OLD TRAFFORD

Emery na vijana wake wataingia katika Uwanja wa Old Trafford ambao umekuwa mgumu kwao kila wanapocheza dhidi ya Manchester United.

Mara ya mwisho Arsenal kushinda kwenye Uwanja wa Old Trafford ilikuwa Septemba 17, 2006 mwaka ambao walitinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Walishinda bao 1-0 lililofungwa na Emmanuel Adebayor.

Miaka 12 imepita tangu waliposhinda ndani ya uwanja huo wanarejea tena leo wakiwa kwenye kiwango kizuri huku wapinzani wao bado hawajakaa sawa tangu kuanza kwa msimu huu. BILA WENGER

Mchezo huo utakuwa wa kwanza kwa Arsenal bila kocha wao, Arsene Wenger ambaye aliitumikia klabu hiyo kwa miaka zaidi ya 20.

Emery ataingia Old Trafford na kucheza dhidi ya Manchester United kwa mara ya kwanza msimu huu ikiwa mpaka sasa Arsenal hawajafungwa michezo 11mfululizo ya Ligi Kuu England. MOURINHO v EMERY

Ni miaka mitano imepita tangu walipokutana mara ya mwisho makocha hao, huku Mourinho akijivunia rekodi ya ushindi mara nne na sare moja dhidi ya Emery wa Arsenal.

Emery bado anasaka ushindi wake wa kwanza dhidi ya Mourinho ambaye anatajwa kuwa na mbinu nyingi wakati wa michezo mikubwa.

Haya ni matokeo ya michezo mitano waliyokutana makocha hao Inter Milan 3-1 Valencia, Real Madrid 2-0 Valencia, Valencia 3-6 Real Madrid, Valencia 2-3 Real Madrid na Real Madrid 0-0 Valencia. KICHAPO KIKALI

Pindi timu hizo mbili kubwa za nchini England zinapokutana mchezo huwa mkali kutokana na kila timu kuhitaji matokeo ya ushindi.

Lakini msimu wa 2011/12 ulikuwa mbaya kwa Arsenal ambao waliingia katika Uwanja wa Old Trafford na kukubali kichapo cha mabao 8-2 kutoka kwa wenyeji wao, Manchester United.

Hicho kilikuwa kipigo kikubwa zaidi kwa Arsenal katika historia yao ya Ligi Kuu England.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.