TUMWELEWE KAKOLANYA, ANAIPIGANIA KESHO YAKE

Dimba - - Dimba -

Ushindi wa michezo minne unawafanya Yanga wabeze mchango wake ndani ya timu, lakini naamini watamtafuta tu. Si kila mchezaji anayegoma anataka kuihama timu. Beno anaitumia Simba ili atimiziwe mahitaji yake Yanga.

ALIWAHI kuniambia rafiki yangu Jonas Mkude kuwa “Mkeyenge mpira ni mchezo wa ajabu sana. Wakati mashabiki wakitoka majumbani mwao kwenda uwanjani kutazama mpira, huziaga familia zao kuwa wanakwenda kupata starehe, lakini sisi (wachezaji) tunaziaga familia zetu kwa kuziambia kuwa tunakwenda kazini.”

Tofauti ya mashabiki na wachezaji inaanzia hapo kwenye mstari huo aliousema Mkude. Sakata la Beno Kakolanya na Yanga limenifikirisha upya juu ya kauli hiyo niliyoisikia kinywani mwa Mkude alipokuwa akipigania mkataba mpya na Simba. Nilimwelewa sana. Tena sana.

Kwa mashabiki kuja uwanjani kwao ni kuja kupata burudani, kisha kurudi majumbani kwao, lakini kwa mchezaji uwanjani ni kazini. Ni sehemu wanayokuja kutengeneza mkate wao wa kila siku. Hawana kazi nyingine za kuingizia siku.

Wachezaji hutengeneza maisha yao kupitia kipindi kama hiki alichonacho Beno. Amejiweka kando na timu. Anataka alipwe mishahara yake na kumaliziwa ada yake ya usajili arudi kazini.

Beno anajua Yanga wameshakuwa mateka wake. Watamtafuta na watakaa chini. Anaamini hili litatokea kama si leo, basi kesho hata keshokutwa. Kiburi kinachowafanya Yanga wasijali malalamiko yake ni kupata ushindi kwenye michezo minne mfululizo. Ila watamtafuta tu!

Kama Beno atashindwa kuitikisa Yanga katika ubora huu unaopatikana katika glove zake hivi sasa, lini tena atafanya hivyo? Kila mmoja ana njia zake za kudai. Beno ameamua kudai kwa kujiweka kando.

Ushindi wa michezo minne unawafanya Yanga wabeze mchango wake ndani ya timu, lakini naamini watamtafuta tu. Si kila mchezaji anayegoma anataka kuihama timu. Beno anaitumia Simba ili atimiziwe mahitaji yake Yanga.

Katika dirisha kubwa la usajili lililopita tuliona jinsi Kelvin Yondani alivyowatumia Simba kupata mkataba mnono Yanga. Mwisho wa siku Yondani alifanikiwa. Beno anatumia njia hii ya Yondani kufikisha ujumbe wake Yanga na kuwakumbusha umuhimu wake kikosini.

Katika hili mashabiki wa Yanga wanapaswa kumwelewa, si kumchukia na kumwona msaliti ndani ya jeshi lao. Beno anajua wazi kama akisajiliwa Simba atakutana na changamoto ya Aishi Manula. Anaondokaje Yanga ambako ni mfalme kisha akaenda sehemu yenye changamoto ya kucheza au kutocheza? Ni ngumu.

Kuna picha nyingi tofauti zinazunguka kichwani mwa Beno. Kuna maisha baada ya mpira. Benno akifikiria maisha baada ya mpira anajiona amesimama katika mstari sahihi wa kufanya hiki anachokifanya.

Kuna mastaa wengi wa zamani tunapishana nao mitaani, tunakutana nao viwanjani wengi wana hali mbaya kimaisha. Hawa ni watu ambao hawakustahili kuishi wanavyoishi leo. Beno akiwaona mastaa hao ndiyo anazidi kujawa hofu na kesho yake.

Yanga hawana ujanja kwa Beno. Itafika muda watamtafuta na hapo Beno ataenda kikaoni kwa mwendo wa madaha. Atatembea kama dume la nyani likiwa na wakeze.

Mikono ya Ramadhan Kabwili na Claus Kindoki ingekuwa salama langoni madai ya Beno yangezidi kupuuzwa zaidi yanavyopuuzwa sasa, lakini mikono ya makipa hao si imara. Beno ataitwa mezani na maisha yataendelea.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.