Ligi Kuu Bara viwanja vitatu kuwaka moto leo

Dimba - - News - NA MAREGES NYAMAKA

WAKATI Simba, Yanga pamoja na Azam FC zikiendelea na michuano ya Mapinduzi kisiwani Zanzibar, Ligi Kuu Tanzania Bara yenyewe haipoi, kwani leo nyasi za viwanja vitatu zinatarajiwa kuwaka moto.

Michezo itakayochezwa leo ni kati ya Biashara United ambao watakuwa uwanja wao wa nyumbani, Karume mkoani Mara kuwakabili Singida United, huku African Lyon wakikipiga katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha dhidi ya Stand United.

Mchezo ambao unatarajiwa kuwa mgumu ni ule wa Kagera Sugar utakaochezwa Kaitaba dhidi ya Mwadui FC.

Msisimko wa michezo yote mitatu inatokana na ukweli kwamba timu nyingi kati ya hizo, zinashika nafasi za mwisho hivyo zitataka kuhakikisha zinashinda ili kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.

African Lyon wanashika nafasi ya pili kutoka mwisho wakiwa na pointi 13, wanatakiwa kuhakikisha wanawafunga Stand United ili kujisogeza mbele kidogo huku Biashara nao ambao wana pointi 13 katika nafasi ya tatu kutoka mwisho wakitakiwa kupata matokeo mazuri mbele ya Singida United.

Akizungumza na DIMBA kocha wa African Lyon, Adam Kipatacho, alisema wamejifunza kutokana na makosa katika mchezo uliopita dhidi ya KMC walipokubali kichapo cha mabao 2-0.

“Tumerejea uwanja wa nyumbani na tumefanya maandalizi mazuri ili kuhakikisha tunachukua pointi zote tatu hapa (Arusha), jambo zuri ni kwamba hatuna mchezaji yeyote aliye majeruhi.

Katika msimamo huo wa ligi, Tanzania Prisons ambao misimu kadhaa imekuwa timu ya kutisha, msimu huu wanaonekana kuwa mteremko kwani wanaburuza mkia wakiwa na pointi 12 huku Yanga wao wakiendelea kutamba kileleni wakiwa na pointi 50.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.