TUMUAGE MARCELO AU BADO YUKO NGANGARI?

Dimba - - Kona -

BEKI bora wa kushoto duniani. Halafu ni raia wa Brazil. Kwa sasa anacheza mpira katika klabu bora duniani, Real Madrid. Huyo ni Marcelo da Silva.

Tena klabu ya karne duniani, Real Madrid. Alijiunga klabuni hapo akitokea kwao Brazil katika timu ya Fluminense.

Anacheza nafasi ya Mbrazil mwingine, Robert Carlos. Akiwa na miaka 18 aliteuliwa kwenye kikosi bora cha msimu cha Ligi Kuu Brazil mwaka 2006.

Ametwaa mataji manne ya Ligi Kuu. Mengine manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alipiga bao kwenye fainali ya mwaka 2014. Akapiga bao katika hatua ya matuta kwenye fainali ya mwaka 2017. Ametwaa taji la mabara na nyingine nyingi sana.

Marcelo amefundishwa na makocha wenye majina makubwa duniani, kama vile Zinedine Zidane, Julen Lopetegui, Santiago Solari, Fabio Capello, Bernd Schuster, Juande Ramos, Manuel Pellegrini.

Amecheza na wachezaji bora duniani kama vile Neymar na Cristiano Ronaldo. Halafu ni shabiki wa klabu ya Botafogo ya kwao Brazil.

Historia ya Marcelo ni kubwa mno katika ulimwengu wa kandanda. Marcelo ni beki ambaye hucheza kama winga. Amekuwa na misimu bora kabisa ndani ya Real Madrid.

Ni fundi, mtaalamu wa pasi, amefunga mabao na mengi mazuri. Akiwa dimbani huwa kama mchezaji wa kila sehemu. Enzi za Zidane unaweza kumwona Marcelo akiwa winga wa kushoto, mshambuliaji, kiungo, lakini ukweli yeye ni beki tatu.

Mojawapo ya mambo yanayowasumbua mashabiki ni namba halisi ya Marcelo. Wakati fulani makocha humpanga kama winga wa kulia. Ndiyo, Zidane alijaribu hii kwa kuwapanga pamoja Theo Hernandez na Marcelo. Wote wawili ni mabeki wa kushoto.

Marcelo ni silaha muhimu ya mashambulizi ya Real Madrid. Tunapita kwa udambwidambwi na kila aina ya ufundi pale tunapompa mpira Marcelo.

Yeye ni silaha inayowasumbua wapinzani. Yeye ni kama vile amepewa mpira ili afunge. Timu nyingi zinapotaka kuifunga Real Madrid wanaanza kumdhibiti Marcelo na mwenzake Dani.

Msimu huu mambo hayakuanza vizuri kwa Marcelo chini ya Julen Lopetegui. Amekumbana na majeruhi kadhaa.

Nilipochungulia taarifa ya klabu yetu hii kuhusu wachezaji waliokuwa majeruhi mara kwa mara ni Marcelo.

Katika rekodi zake zinaonyesha kuwa Marcelo amekosa mechi 6 za Ligi Kuu Hispania. Amekosa mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Marcelo amekosa mechi mbili za Cope Del Rey. Majeraha ya mara kwa mara yamerudisha nyuma ari na kiwango cha Marcelo.

Kila awapo uwanjani haonekani kuwa timamu kimwili. Ufundi wake ungalipo, lakini uimara na udambwidambwi ni kama vile umepungua.

Tukifanya uchunguzi wa awali tunagundua tatizo ni majeraha. Uchunguzi zaidi utatufikisha kujiuliza, je, tumefika mwisho wa kuona umahiri wa Marcelo? Ngoja kidogo, kwanza ana miaka 30. Ni mkongwe. Mzoefu.

Mhenga na maneno mengine yanayomfaa. Kwa umri wake unaona kuwa Marcelo hawezi kuwa yule aliyewatandika bao tamu watani wetu wa jadi, Atletico Madrid pale jijini Lisbon nchini Ureno. Marcelo hawezi kuwa yule aliyewatetemesha Juventus pale jijini Cardiff nchini Wales kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2017. Marcelo si yule aliyemwaga machozi mwaka 2016 baada ya kupiga penalti maridadi dhidi ya walalahoi Atletico Madrid. Marcelo huyu si yule aliyemimina majalo matamu kwa Gareth Bale kabla ya kupiga tikitaka ya kumtungua golikipa wa Liverpool msimu uliopita. Ni wazi tunaweza kupata ubora wa Marcelo kwa misimu mingine miwili au mitatu. Lakini ubora huo hautakuwa kama awali. Kwa hiyo utaona Marcelo kwa umri wa miaka 30 sasa hawezi kuwa na kasi au kufanya mambo makubwa kama zamani. Mwili wake umeanza kumgomea. Msimu huu tunaona sura ya majonzi ya Marcelo si ile ya kushangilia ushindi uwanjani. Tunamwona Marcelo ambaye anahuzunika. Analia, anafuta kamasi na machozi. Mwili unazidi kumgomea. Nguvu zinazidi kumwishia. Sasa tutafanyeje, tuendelee hivi au tumuage kabisa Marcelo wetu kipenzi? Tunaanzia wapi kwa mfano? Mabosi wetu wa kikosi cha Real Madrid wanayaona machozi ya Marcelo ndiyo maana ilikubaliwa mapema kijana wetu wa Castilla, Sergio Reguilon, apandishwe. Katika mechi karibu zote alizokosa Marcelo tumeona kipaji kingine. Hiki ndicho kinaitwa Sergio Reguilon. Ni beki wa kushoto aliyechangia kuondolewa kwa Theo Hernandez na kupelekwa Real Sociedad kwa mkopo.

Wakati tunafurahi kipaji cha Reguilon, mimi akili haijakaa sawa. Nafikiria ubora Marcelo namna unavyotoweka. Akifikisha miaka 33 bado hatakuwa kama yule wa miaka 24 hadi 28.

Umri wa miaka 33 ndio uliomng’oa Roberto Carlos. Ni umri wa kutafuta pensheni. Sitashangaa kuona Marcelo akiagwa Real Madrid. Itahuzunisha lakini ukweli lazima tukubali kuwa Marcelo hatakuwa kama tulivyozoea.

Viungo vya mwili wa mwanadamu huwa vinakataa kufanya kazi. Tuliona hilo kwa akina Marco van Basten. Tuliona hilo kwa kijana wetu Fabio Coentrao.

Marcelo wa sasa anatumia muda kumnoa Sergio Reguilon. Kijana huyu anakuja vizuri na atakipiga zaidi klabuni.

Inasikitisha kuona Marcelo atakapokuwa nje ya viwanja vya soka. Ukweli lazima tuubebe sasa, tumwage Marcelo au tuamini atakuwa ngangari kwa asilimia 100?

Muda utaongea.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.