DORTMUND

INAPOENDELEA KUTUPA SABABU ZA UTAWALA WA

Dimba - - Dimba Special -

HERI ya mwaka mpya kwa wasomaji wote wa ukurasa huu wa Penalti ya Mwisho, ikiwa hii ni ya kwanza ndani ya mwaka huu tena kwa matumaini makubwa Mungu aendelee kutupa baraka na mafanikio tele.

Katika tasnia ya michezo kuna mambo mengi yalitokea ndani ya mwaka uliopita kwa kiasi fulani wapo waliofurahi na wengine haikuwa hivyo kwao, lakini hilo halina nafasi tena mwaka huu.

Kila mmoja wetu anatamani kuona mabadiliko yenye tija na faida kwa nchi yetu yakipewa kipaumbele zaidi kuliko yaliyokithiri kubomoa hiki kilichopo.

Tuachane na hilo kidogo, hivi ushaiangalia Borrusia Dortmund vizuri tangu kuanza kwa msimu huu?

Labda inawezekana unaifuatilia sababu inaongoza Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga tena wakiwaweka Bayern Munich kwenye wakati mgumu.

Au hata kama huifuatilii lazima taarifa zao zitakuwa zimepenya kwenye ngoma za masikio yako au kuonekana mbele ya mboni za macho na kujua ni kipi kinaendelea kwao.

Ligi hiyo bado haijamalizika, tayari Borrusia Dortmund wameonyesha dalili za kutwaa taji hilo msimu huu baada ya Bayern Munich kulichukua kwa zaidi ya misimu mitatu mfululizo.

Safari bado ni ndefu sababu chochote kinaweza kutokea na kukatisha matumaini yaliyojaa kwenye maono ya mashabiki wa Borrusia Dortmund kuhusu kushinda taji hilo msimu huu.

Kwa kiasi kikubwa Borrusia Dortmund wamekuwa wakitoa changamoto kubwa kwa Bayern Munich ndani ya Bundesliga lakini hawana mwendelezo mkubwa kiasi hicho.

Kipindi cha Jurgen Klopp walifanikiwa kutwaa taji la Bundesliga mara mbili mfululizo huku wakifungwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na wenzao Bayern Munich ndani ya Uwanja wa Wembley.

Najua unajiuliza kwanini Borrusia Dortmund wanashindwa kuishi kwenye utawala kwa muda mrefu kama miaka mitano au zaidi?

Basi iko hivi, siku tatu au nne zilizopita Borrusia Dortmund walimuuza Christian Pulisic kwa ada ya pauni milioni 57 kwenda Chelsea.

Ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimetolewa na hatimaye kuwashawishi Borrusia Dortmund kumtoa nyota huyo raia wa Marekani. Ili uwe timu bora lazima uwe na wachezaji walio na ubora mkubwa ndani ya kikosi chako, unadhani Borrusia Dortmund hawana nyota wenye ubora?

Labda itakuwa umejiuliza hivyo! Lakini maana kubwa ya Borrusia Dortmund kushindwa kutawala soka la Ujerumani na Ulaya ni kuondoka kwa wachezaji tegemeo na wenye ubora ndani ya kikosi hicho.

Jaribu kufikiri kama wangekuwa na nyota wao wote, labda ni kipi kingetokea? Naamini umetengeneza picha ndani ya ubongo wako na kutikisa kichwa kwa hatari iliyotakiwa kuwepo ndani ya kikosi cha Borrusia Dortmund.

Ukimtoa Pulisic, miaka ya hivi karibuni walifanya biashara ya kuwauza Henrink Mkhitaryan, Pierre-Emerick Aubameyang, Robert Lewandowski, Ousmane Dembele, Mario Gotze ambaye amerejea kwa mara nyingine.

Ni wachezaji wa daraja la juu wenye uwezo na ubora mkubwa, lakini hivi sasa wanatumika klabu nyingine.

Nakitazama kikosi hiki cha sasa cha Borrusia Dortmund kwa jicho la biashara zaidi kwao kuliko mafanikio na kuandika historia kubwa Ujerumani na Ulaya.

Kijana mdogo, Jadon Sancho, si muda mrefu utasikia anahitajika na timu za Barcelona, Real Madrid, Manchester United na klabu nyingine zenye uwezo mkubwa zaidi. Ni ngumu kumtoa mchezaji wa kikosi cha kwanza ndani ya kikosi cha Bayern Munich, Real Madrid au Barcelona labda mchezaji mwenyewe aamue kuondoka au klabu isimwongezee mkataba.

Mpaka leo hii ndani ya kikosi cha Bayern Munich unawaona akina Arjen Robben, Frank Ribery, Thomas Muller, Jerome Boateng, Manuel Neuer na David Alaba.

Hao ni wachezaji wenye uwezo mkubwa na bora ambao wapo ndani ya timu hiyo kwa zaidi ya misimu mitano kwa pamoja na huo ni msingi au uti wa mgongo wa kikosi cha Bayern Munich.

Achana na akina Thiago Alcantara, James Rodriguez, Robert Lewandowski na wengine wenye ubora mkubwa wameingia kikosini misimu ya hivi karibuni na usitegemee kuona wakiondoka kwa urahisi ndani ya timu hiyo.

Upande wa Borrusia Dortmund umekuwa utamaduni wao kuuza nyota wao wakati mwingine inaaminika uchumi hafifu unasababisha hilo kutokea.

Tayari wameanza kwa kumuuza Pulisic kwenda Chelsea na kuna uwezekano mkubwa wengine wakafuata kama si mwisho wa msimu huu au hata ujao, yaani hawana uhakika na wachezaji wao.

Kwa tabia hiyo ni ngumu kwa Borrusia Dortmund kuvunja utawala wa Bayern Munich na hakuna dalili zozote zinazoonekana hilo kutokea.

Kwa urahisi tu, Borrusia Dortmund wanaendelea kutupa sababu za Bayern Munich kuendelea kuwa watawala wa Ujerumani kwa muda mrefu zaidi labda itokee misimu kadhaa kama ilivyokuwa au ilivyo hivi sasa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.