VIGOGO SIMBA WATETA NA 'MO' KUWAMALIZA WAARABU

Dimba - - Mbele - NA MWANDISHI WETU

VIONGOZI wa klabu ya Simba chini ya Mwekezaji Mkuu, Mohamed Dewji 'Mo', jana walikutana katika kikao maalumu ambapo ajenda kubwa ilikuwa ni mechi ya timu hiyo dhidi ya JS Saoura ya Algeria.

Kabla ya kikao hicho, Mo, alikutana na Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Ausemss na kujadili masuala kadha ya kiufundi na sasa amemalizia na vigogo wenzake kwa ajili ya kuweka mambo sawa.

Habari ambazo DIMBA limezipata kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kwamba, vigogo hao kwa pamoja wameazimia kuingia vitani kuhakikisha Waarabu hao hawatoki katika mchezo huo utakaopigwa Januari 12, jijini Dar es Salaam.

Simba wapo Kundi D katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika sambamba na Al Ahly ya Misri, AS Vita ya Congo pamoja na JS Saoura ya Algeria ambao ndio watakaoanza kucheza nao mchezo huo unaokuja.

Kwa mujibu wa mjumbe aliyelipenyezea gazeti hili habari kutoka ndani ya kikao, amesema pamoja na mambo mengine lakini kikosi kazi cha Simba kimeshawachunguza vya kutosha Waarabu hao na kwamba wana uhakika wa kushinda mechi hiyo ijayo.

Habari zaidi zinasema tayari kocha wa Simba ameshakabidhiwa baadhi ya nyenzo za kuifahamu timu hiyo kama vile mikanda ya mechi mbalimbali na pia majina yote ya wachezaji pamoja na wasifu wao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.