Buriani Mgonahazelu 'kete ya mwisho' Vijana Jazz

Dimba - - Nyuz Nyuz - JIMMY CHIKA [email protected] 0712 328 223 Mungu ailaze mahala pema peponi roho yake...Amina.

KWA sasa unaweza kuliita jina lake ukianzia na neno marehemu Abdalah Mgonahazelu, inauma sana.

Ni mwanamuziki nguli wa bendi ya Vijana Jazz ambaye baada ya kutoweka duniani kwa idadi kubwa ya wenzake katika kundi hilo, yeye alibaki kama alama ya bendi, lakini naye leo hayupo tena.

Vitabu vya dini vingi vinatuasa kuwa tunapompoteza mwenzetu katika uso wa dunia, tusifikirie alitoka wapi bali tuiombee safari yake iwe ya heri, nasi tutazidi kumwombea Mgonahazelu.

Jina hili lilianza kupenya kwenye masikio ya wapenzi wa muziki si kutoka katika bendi ya Vijana Jazz, la hasha bali kundi la Madevela Sound ndilo hasa lililoanza kutangaza kipaji chake.

Akiwa na kundi hilo miaka ya kati ya 1980 sina hakika miezi, alirekodi nyimbo kadhaa ukiwemo Baba watoto, ambapo yeye marehemu aliutunga na kisha kuuimba yeye na kaka yake Majuto Mbugani.

Walipokezana vizuri katika uimbaji kiasi cha kumshawishi aliyekuwa kiongozi wa Vijana Jazz, hayati Hemed Maneti Ulaya, kumkubali Mgonahazelu ajiunge na bendi hiyo na kumwingiza katikati ya waimbaji nguli waliokuwepo kundini.

Alianza kuonekana nuru katika bendi hiyo kutokana na uwezo wake wa kuziba nafasi nyingi pindi anapotokea mwimbaji fulani hakuwepo kundini.

Kuna wakati aliimba sehemu alizoimba marehemu Maneti mwenyewe, wakati mwingine aimbe vipande vya Selemani Mbwembwe na akafanya hivyo hivyo kwa sauti za marehemu Jerry Nashon, Said Hamisi, Mohamed Gotagota, Fred Benjamin, Suleyman Mbwembwe na hata nyimbo alizokuwa akiimbisha kiongozi wa bendi ya Kamanyola kwa sasa Benno Villa, Antony Maghali.

Kwa ujumla maisha yake katika tasnia ya muziki aliyakabidhi Vijana Jazz, ikawa yeye ndiyo alama ya bendi hiyo kutokana na kutoihama tangu alipojiunga mwaka 1990.

Si rahisi kujua idadi ya nyimbo alizoshiriki kurekodi, lakini ni idadi kubwa, kwani alikuwa mwimbaji tegemeo hasa anapoimba sauti

kwanza, lakini pia alikuwa mtunzi mwenye sifa stahiki.

Endapo utatamani kuisikia vizuri sauti yake ili uifahamu, basi tafuta wimbo uitwao Baemade ambao humo alilalamika vya kutosha kuwatetea wafanyakazi hiyo wasinyanyaswe.

Lakini leo hii unapohesabu safu ya uimbaji iliyodumu kutokea miaka hiyo ya 90 hadi leo, unaweza kusema Mgonahazelu ndiye aliyekuwa kete ya mwisho pale Vijana Jazz.

TUKIO NILILOMFANYIA STUDIO

Sikumbuki mwaka wala tarehe, lakini siku hiyo tulikutana katika studio za TBC FM pale Barabara ya Nyerere, mimi nilialikwa kwa ajili ya uchambuzi na yeye marehemu alikuwa mgeni wetu.

Mwandaaji na mtangazaji alikuwa ni Camarader Hassan Mbazigwa na mimi nilialikwa kama mchambuzi.

Mwongozaji wa kipindi akanipa taarifa kwamba, punde tutakuwa na wageni wawili kutoka Vijana Jazz, marehemu Mgonahazelu na mwenzake, Saburi Athumani.

Niliposikia ugeni huo haraka sana nikamwomba Mbaziugwa atafute wimbo wa Baba watoto, nikiwa na uhakika kwamba ndiyo kazi yake ya kwanza kuirekodi katika historia yake ya uanamuziki.

Naam, hiyo tukaifanya siri yetu mimi na mtangazaji na walipoingia tukawakaribisha na tukaongea mengi kuhusiana na bendi yao ya Vijana Jazz.

Lakini ilipofikia wakati wa kupata burudani, ndipo tulipoonyeshana ishara na kuanza kupiga kibao hicho.

Lilikuwa ni tukio lililomshitua sana Mgonahazelu, akashikwa na furaha iliyopitiliza na kumfanya akumbuke mengi katika maisha yake.

Lakini akalalamika kwamba tukio kama lile lingeweza hata kumwangusha chini kwa presha maana hakutegemea!

ABDALAH MGONAHAZELU

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.