Siri za Waalgeria zatua Msimbazi

Dimba - - Mbele - NA SAADA SALIM

WAKATI kikosi cha JS Saoura, kikitarajiwa kuwasili nchini kesho, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amesema amewatumia marafiki zake wanaoishi nchini Algeria kujua mbinu za wapinzani wao hao.

Simba watakuwa wenyeji wa Waarabu hao, mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ya wiki hii Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Aussems alisema licha ya kuwafuatilia wapinzani wao hao kwa njia ya mikanda ya video, lakini pia aliwatumia marafiki zao ambao nao hawakumwangusha, kwani walimweleza kila kitu.

“Nimefanikiwa kuwatumia watu wangu wa karibu kupata taarifa zao, kwa ujumla tunafanyia kazi kila ambacho tunahisi kitatusaidia kupata matokeo mazuri katika mchezo wetu huo wa kwanza kabisa uwanja wa nyumbani.

“Nimefuatilia kuhusu michezo yao ya hivi karibuni waliyocheza ili tu kujua namna ya kukabiliana nao. Ukitaka kupambana vizuri na adui yako lazima ujue kwanza aina ya silaha anayoitumia,” alisema.

Moja ya michezo ambayo huenda Aussems aliifuatilia kwa umakini mkubwa ni ule ambao wapinzani wao hao walikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa JS Kabylie, mchezo wa Ligi Kuu nchini Algeria.

Akizungumza kuhusu kukosekana kwa Erasto Nyoni, aliyepata majeraha kwenye michuano ya Mapinduzi, alisema nafasi yake itazibwa vizuri, kwani anao vijana makini kama Jjuuko Murushid, Paul Bukaba pamoja na Yusuph Mlipili.

Baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya kujiwinda na mchezo huo wa Jumamosi dhidi ya Waarabu hao na kuwaachia wengine kuendelea na michuano ya Mapinduzi, ambapo wametinga hatua ya nusu fainali.

MAPINDUZI CUP

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.