SIMBA SC INA JIPIGIA TU MAPINDUZI ZENJI

Dimba - - Mbele - NA SAADA AKIDA,ZANZIBAR

BAO la dakika 21 lililofungwa na kiungo wa kimataifa wa Simba Haruna Niyonzima lilitosha kuifanya timu hiyo kumaliza kibabe hatua ya makundi michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya jana kuichapa Mlandege, mchezo uliopigwa uwanja Amaan mjini Zanzibar.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kwa timu zote kujaribu kupanga mashambulizi ya hapa na pale lakini iliwachukua Simba dakika 21 kupata penalti baada mwamuzi wa kati Rashid Farhan kuamuru kupigwa adhabu hiyo kutokana na Ali Hamduu kumuangusha Asante Kwasi katika eneo la hatari.

Huo ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Simba kwani walianza Kombe la Mapinduzi kwa kuinyuka KMKM bao 1-0, kabla ya kuvuna karamu ya mabao 4-1 dhidi ya Chipukizi.

Dakika 33 ya mchezo huo Mlandege walipata pigo baada ya beki wao mahiri Hamduu kuumia goti na kukimbizwa hospitali huku nafasi yake ikichukuliwa na Fini Salum

Bao hilo lilidumu hadi mapumziko ambapo kipindi cha pili timu hizo zilifanya mabadiliko kwa Simba kumtoa Nicholas Gyan nafasi yake ikachukuliwa Zana Coulibaly, Jjuuko Murshid/ Paul Bukaba na Jonas Mkude/ Said Ndemla.

Kwa upande wa Mlandege Yahya Haji alitolewa nje na nafasi yake ikachukuliwa na Said Khamis.

Dakika 54 almanusura Mlandege wasawazishe bao hilo kupitia kwa Said Khamis ambaye alipiga shuti likadakwa na kipa Deo Munishi.

Simba walijibu shambulizi hilo dakika ya 63

kwa Adam Salamba kupoteza nafasi ya wazi baada ya mpira kukolewa Abubakar Ame wa Mlandege.

Dakika ya 71 Said Khamis alilitia tena msukosuko katika lango la Simba baada ya kupiga krosi murua lakini mpira ukatoka nje ya lango.

Aidha Simba walikosa bao la wazi dakika 78 kupitia kwa Shiza Kichuya baada ya shuti lake kupaa juu ya lango la Mlandege na kutoka nje.

Anderson Charles alipiga krosi kwenye lango la Simba dakika 81 lakini mpira ukatoka nje kabla ya Wekundu wa Msimbazi kupoteza nafasi ya kufunga dakika ya 83 kwa Niyonzima kupiga shuti na mpira kuwa kupaa juu ya goli.

Hadi mwisho wa mchezo Simba walitoka kifua mbele kwa ushindi wabao hilo, hivyo kusubiri mchezo kati ya Malindi na Azam kujua timu watakayoumana katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.