Yanga msifanye makosa

Dimba - - News -

KAMPENI za wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika klabu ya Yanga, zilianza jana kwa kuwakutanisha wagombea na wanachama kwa ajili ya kunadi sera zitakazoshawishi kuwapigia kura.

Uchaguzi huo utafanyika Januari 13, zikiwa zimebaki takribani siku tano, hiyo ni dhahiri kwamba tayari klabu hiyo imefikia wakati wa kupata uongozi wake na kuondokana na sintofahamu iliyotamalaki klabuni hapo kwa kipindi kirefu.

Miongoni mwa nafasi muhimiu zinazogombewa ni uenyekiti ambao hadi zoezi hilo linaanza ni majina mawili tu, Baraka Igangula na Jonas Tiboroha ndiyo watakaopambana kuwania nafasi hiyo kubwa ya uongozi.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti angalau majina mengi ya wanachama yamechomoza, akiwemo Pindu Luhoyo, Titus Osoro, Salum Magege Chota na Yono Kevela.

Sisi DIMBA tunawakumbusha wanachama wa Yanga kuwa makini katika kipindi hiki ili wazisikilize sera huku wakiwatafakari wanachama hao wenzao wanaoomba uongozi, huku wakijua kwamba wanawakabidhi mustakabali mzima wa klabu yao.

Uzoefu wetu katika masuala ya uchaguzi hasa katika klabu hizi mbili kubwa zenye idadi kubwa ya wanachama, Simba na Yanga unaonyesha mara nyingi wanachama huchagua kwa kukurupuka na baadaye kuanza kujilaumu kwa makosa waliyofanya.

Ndiyo maana tunasisitiza kwamba, hiki ni kipindi kizuri kwa kufanya tathmini na hasa kuwachagua wanachama wanaosema na kuonyesha sura ya kweli yenye machungu ya kuisaidia klabu hiyo.

Tunawakumbusha kwamba mwenendo wa klabu hiyo hadi sasa uko vizuri hasa katika ushiriki wa Ligi Kuu, ni kutokana na kuwa na rasilimali watu ambao baadhi yao wamekuwa wakijitoa kuisaidia timu, lakini vinginevyo hali ingekuwa tete.

Ni kwa muktadha huo tu, DIMBA tunarudia kuwasihi wanachama wafanye upembuzi bila kujali mshindo wa ngoma wala ahadi za Abunuwasi, kwani vinginevyo midomo waliyoitumia kucheka, kesho itawasaidia kulia. Tunawatakia wagombea wote kampeni njema na zenye ustaarabu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.