MAUA SAMA

mwanadamu anaishi mara moja

Dimba - - Sultan - NA ABDULAH MKEYENGE

KABLA ya wimbo wa Iokote sikuwa nikimjua msanii, Maua Sama. Hata ningepishana naye mtaani nisingethubutu kugeuza shingo yangu kumtazama tena. Ningejiona kama nimepishana na mdada mmoja mrembo. Maisha yako kasi sana. Leo Maua ndiyo staa wa Bongo Fleva.

Hivi sasa nitakuwa mnafiki nikisema simjui yeye wala wimbo wake. Ni Maua aliyetuletea wimbo wa Iokote uliotuteka kwenye ngoma zetu za masikio. Ni Iokote inayobamba kumbi za starehe, nyumbani na vituo vya kurushia matangazo. Imeshika sehemu nyingi.

Kwa takwimu zangu zisizo rasmi huu ndiyo wimbo unaosikilizwa mara nyingi zaidi na wasikilizaji wengi kwa kutwa nzima. Kituo kipi cha redio hivi sasa kinaweza kupiga nyimbo tano bora bila kupiga na wimbo wa Maua? Jibu la haraka ni hakuna! Maua amekuwa mkubwa ghafla. Nasikia hata wasanii wenzake wanamheshimu sana siku hizi.

Hawamchukulii kama walivyokuwa wanamchukulia zamani. Katika ukubwa huu wake anapaswa kufahamu kitu kimoja kikubwa. Kitu chenyewe ni mwanadamu kuishi mara moja tu. Haishi mara mbili.

Katika muda huu ambao Iokote imekuwa kubwa kuliko jina na sura yake, anatakiwa kuziokota kweli fedha. Azikamue na kuzichuma fedha zote zilizoko mbele yake. Muziki wa Bongo hautabiriki sana siku hizi.

Hiki ndicho kipindi cha kubadili maisha yake kiujumla. Kama hatabadili maisha kupitia Iokote, atachukua muda mrefu kubadilika. Sitaki niwe mtabiri katika hili, lakini Iokote inatakiwa kubadili kila kitu cha Maua.

Kuna wasanii wamewahi kutoa wimbo ulioshika kama huu. Wakawa wanaogelea fedha. Hawa walikuwa matajiri wakubwa. Lakini hawakuishi kwa kuitazama kesho. Walifuja fedha na mali zao.

Walilala kumbi za starehe. Walijiona wamemaliza mwisho wakaangukia katika dimbwi la ubwiaji dawa za kulevya. Hivi leo mitaani wamekuwa ombaomba mashuhuri na wataja majina ya waliofanya wafikie hapa walipo. Mchawi wa kwanza wa mwanadamu ni mwanadamu mwenyewe.

Natamani kukutana na Maua. Natamani sana. Lakini natumai andiko hili litamfikia popote pale. Wasia wangu kwake ni mmoja tu. Aitumie Iokote kufanya mambo makubwa kabla mtaani hakujatokea wimbo mwingine wa kushika masikio ya wasikilizaji.

Nyimbo nyingi za mdogo wangu William Nicholaus ‘Bill Nass’, zinafanya vyema mitaani, disko, runingani na redioni. Lakini katika maisha yake ya sanaa hajawahi kupata wimbo wa kubadili maisha yake kama Iokote. Anapata wimbo wa kumfanya auze gari lake Mark X, aongezee fedha kidogo anunue gari jipya Crowun. Amegotea hapo.

Maua anaweza kuifanya Iokote ikampeleka mbali. Lakini kama akifanya mzaha katika kipindi hiki, usiku mmoja ndani ya kitanda chake nyumbani akiwa mwenyewe anaweza kulia sana. Atalia na mengi. Atazikumbuka nyakati zake nzuri Iokote ilipokuwa inafanya vyema.

Sasa kabla mambo hayajafikia huko, aitazame kesho yake ili tuje kumtaja kama moja ya wasanii mahiri waliotumia sanaa ya muziki kuwa tajiri mkubwa. Na asiwe kama wasanii wanaoranda mitaani wakiwa na lundo la lawama ambazo haziwasaidii kwa sasa.

NA ABDUL MKEYENGE

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.