Coulibally atatuumbua au yale yale ya Chirwa na Pape Ndaw?

Dimba - - Sultan - NA MAREGES NYAMAKA

SIMBA tayari wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, baada ya kushinda michezo miwili mfululizo kabla ya jioni ya jana kuhitimisha hatua ya makundi. Chipukizi kutoka Pemba walikuwa wa kwanza kuonja joto ya jiwe wakipokea kichapo cha mabao 4-1 kabla ya mwishoni mwa wiki KMKM kutunguliwa bao 1-0 katika kundi A.

Katika mchezo huo wa pili, kikosi cha kwanza Simba kilikuwa na jumla ya wachezaji watano, Pascal Wawa, Zana Coulbally, James Kotei, Clatous Chama pamoja na Mganda, Emmanuel Okwi.

Meddie Kagere na Asante Kwasi wao walikuwa jukwaani kama watazamaji, wakiwa na mapumziko maalumu kutoka kwa kocha wao, Patrick Aussems, baada ya kupewa nafasi ya kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Chipukizi FC.

Kiwango cha beki wa kulia, Coulibally, bado kiliendelea kutoa taswira mbili tofauti. Kupitia katika nyayo za Mzambia, Obrey Chirwa akiwa Yanga au za Pape Ndaw aliyewahi kuitumikia

Simba kwa muda mfupi.

Unajiuliza imekuwaje nimewataja wawili hao? Chirwa alitumia muda wa kutosha kuzoea mazingira na falsafa nzima ya Yanga kabla ya kuanza kung’ara tofauti na alivyochukuliwa awali alipowasili mahali chini ya kocha, George Lwandamina.

Mzee Ibrahim Akilimali mwenye Yanga yake alikuwa mstari wa mbele kumshambulia Chirwa, kuwa alikuwa mchezaji wa kawaida mno akisahau katika soka kuna aina mbili za wachezaji ndani ya makazi mapya. Kwanza mhusika kung’ara moja kwa moja kama walivyokuwa kina Thabani Kamusoko, Feisal Salum wote Yanga, Justice Majabvi (Simba), lakini kundi la pili ni mchezaji apate muda wa kutosha ndicho kilichotokea kwa Chirwa. Akamuumbua Akilimali na wenye mtazamo kama yeye. Chirwa ameondoka Yanga akiwa ni mfungaji bora. Klabu ikimhitaji kuliko yeye alivyokuwa akihitaji kuhudumu mahali ambapo kulikuwa kumeyumba kweli kiuchumi.

Lakini ukigeukia upande wa pili kilichotokea kwa Msenegal, Ndaw, mchezaji wa kigeni ambaye moja ya maajabu yake ni kuamini ubora wake ungechagizwa na viatu vilivyochakaa. Alifeli kweli.

Turejee kwa Coulibally. Hana utulivu uwanjani, miguu yake inapapara sana, krosi zake hazijafikia hata robo ya zile za Shomari Kapombe, kukaba kwake ni nadra kumwacha salama mpinzani, harudi eneo husika kwa wakati. Tatizo, likianza kwake hana uwezo wa kulitatua.

Utimizaji wake wa majukumu kwa usahihi umekuwa tofauti na Mzambia Clatous Chama, Mrwanda, Meddie Kagere ambao pia ni msimu wao wa kwanza.

Si dhambi mchezaji kushindwa kung’ara kwa wakati kuliko matarajio ya wengi kila kukicha linatokea hilo duniani kote, mbaya zaidi ni pale pale atakapofeli kabisa kama ilivyokuwa Laudit Mavugo ndani ya misimu miwili.

Mavugo yule wa Vital’O aliyekuwa moto kwenye ligi ya kwao akifunga mabao 30 ndani ya msimu mmoja, lakini mambo yalikuwa tofauti kabisa akishindwa kufunga hata mabao 10 katika msimu mmoja akiwa Simba.

Kiwango cha beki wa kulia, Coulibally, bado kiliendelea kutoa taswira mbili tofauti. Kupitia katika nyayo za Mzambia, Obrey Chirwa akiwa Yanga au za Pape Ndaw aliyewahi kuitumikia Simba kwa muda mfupi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.