UBUNGE WA KIPA TP MAZEMBE KIPO CHA KUJIFUNZA

Dimba - - Mbele - ONGO

DR imepata Rais mpya. Huyu si mwingine ni Felix Tshisekedi ambaye amembwaga mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu.

Mshindi huyo wa kiti cha urais pia alimgaragaza mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na Serikali ya Rais Joseph Kabila, anayemaliza muda wake, Emmanuel Shadary.

Kwa wafuatiliaji wa masuala ya siasa kwao habari kubwa iliyotawala vichwani mwao ni mpinzani kumshinda mgombea wa chama tawala.

Kwetu familia ya michezo stori kubwa iliyopamba uchaguzi wa Congo ni ushindi wa kiti cha ubunge kwa kipa wa zamani wa klabu ya TP Mazembe, Robert Kidiaba Muteba.

Kipa huyo maarufu kwa ushangiliaji wake wa kuruka kichura chura enzi zake akiwa langoni ametwaa Ubunge wa Jimbo la Upper Katanga nchini Congo DR kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (NPDD).

Kidiaba mwenye miaka 42, alistaafu soka ya ushindani mwaka 2015 na kujikita kwenye masuala ya siasa kabla ya kuibuka kidedea mbele ya wagombea wenzake kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi huo.

Ushindi wa Kidiaba unatupa somo kwamba kumbe umaarufu wa soka unaweza kuwa daraja la kuanzisha maisha mengine nje ya soka.

Kidiaba alifanikiwa kung'ara na TP Mazembe kwenye mataji iliyovuna ndani ya Congo na yale ya kimataifa. Akatumia fursa kuandaa maisha mengine kwa kujipenyeza kwenye siasa.

Kwa Afrika, Kidiaba si mwanasoka wa kwanza kujichomeka kwenye siasa na kuula. Kuna mtu anaitwa George Opong Weah, ambaye kwa sasa ni Rais wa Liberia. Umaarufu wake ulitokana na soka.

George Weah aliwika na klabu za Monaco, Paris St-Germain na AC Milan akikaa muda mfupi Chelsea na Manchester City na kufanikiwa kuwa mchezaji wa kwanza wa soka kutoka Afrika kushinda tuzo ya mchezaji bora wa (Fifa).

Ikumbukwe Weah baada ya kustaafu soka la ushindani aliingia kwenye siasa za Liberia na kukumbana na mizengwe ya kukosa elimu ya shahada na kulazimika kurudi shule kusoma kabla ya kutwaa urais.

Kwetu Tanzania wapo wanasoka waliowahi kuwika lakini baada ya kustaafu soka wakajipenyeza kwenye siasa na kuchomoza kivingine.

Rejea kwa kocha msaidizi wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars marehemu, Joel Bendera. Aliingia katika siasa kama Mbunge wa Korogwe akawa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Kwa nyakati tofauti akawa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Manyara

Ni maisha ya soka yaliyomuwezesha kupata umaarufu wa kuvuna nafasi zote za utumishi serikalini.

Achana na Bendera watupie jicho Mbunge wa zamani wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage ambaye umaarufu wake ulitokana na soka enzi akiichezea Simba na baadaye kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo kabla ya kujielekeza kwenye maisha ya siasa.

Mtazame beki wa zamani wa Simba, Abdul Mteketa ambaye aliukwaa ubunge wa Jimbo la Kilombero mwaka 2010 kabla ya kupoteza nafasi hiyo lakini yupo mtu anaitwa Venance Mwamoto ambaye ni mchezaji wa zamani za klabu za Kihesa Stars, Lipuli ya Iringa, RTC Kagera na Majimaji ya Songea.

Hili ni somo kubwa ambalo Kidiaba anawapa baadhi ya wanasoka wenye kuwika sasa Tanzania kama Mbwana Samatta, Simon Msuva na wengineo kutoogopa kuchungulia fursa za kisiasa siku za usoni.

Kama iliwezekana kwa wanasoka wengine basi hata na kwao kuwaona wakiwa wabunge hata nafasi ya urais ni jambo jepesi kama wataanza kujichongea barabara sasa kupitia umaarufu walionao.

Mbali na ubunge, Kidiaba bado hajaliweka soka kando kwani ni Kocha Msaidizi wa TP Mazembe ambayo aliisaidia kushinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.