VIRAKA SI SULUHISHO LA KUDUMU

Dimba - - Kona ya ubuyu -

URUALI ikitoboka unaweza kupeleka kwa fundi aweke kiraka. Akimaliza kuweka kiraka hicho, mwenyewe unafurahi, unafarajika na kudhani umetatua. Lakini ukweli ni kwamba, viraka hivyo si suluhisho.

Suruali hiyo inapokuwa na matundu mengi kisha ukaendelea kumpelekea fundi akuwekee viraka, basi hilo si suluhisho la kudumu la kulinda mwili wako. Kama viraka vinazidi mwonekano wa suruali basi hata fundi mwenyewe atakushauri ununue nyingine ambayo itakaa muda mrefu kusitiri mwili wako.

Nataka kusema nini? Timu yoyote duniani lazima ikutane na changamoto. Timu yoyote duniani lazima ikabiliane na wapinzani wakali au wenye kiwango cha chini. Kwa hiyo linapokuja suala la kusajiliwa wachezaji ni lazima liangaliwe kwa umakini, wanasajiliwa ili kufanya nini? Ili wawe viraka au suluhisho la muda mrefu.

Namaanisha nini? Kusajili wachezaji ili kuziba pengo la mchezaji aliyehama katika timu yako hakuna tofauti na kuweka viraka kwenye suruali. Kufikiria usajili wa mchezaji fulani aje kuziba pengo la fulani katika klabu yetu, hiyo si sawa kabisa.

Kwenye timu yetu viraka kama Gabreil Heinze walikuwepo, lakini hawakusaidia kitu kama suluhisho la kudumu la Marcelo Vieira da Silva. Kiraka hakikudumu, kikatupwa jalalani. Lakini Marcelo aliyekuwa suluhisho la kudumu ameleta mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Uongozi makini katika taasisi yoyote unafahamu kuwa suluhisho lake si kuweka viraka bali kununua nguo ambayo italinda hadhi kwa muda mrefu.

Kama shabiki wa Madrid anafikiria kumsajili mchezaji wa kuziba pengo la Cristiano Ronaldo, basi hana tofauti na mtu anayepeleka suruali yake kwa fundi kuziba viraka.

Mara nyingi anayependa kuziba viraka anajifariji kuwa heri viraka hivyo vinasaidia kumsitiri wakati inaonekana wazi alichovaa hakina tofauti na rapurapu.

Ndiyo maana mtu kama Juni Calafat kwa sasa ametuletea Vinicius Junior na Rodrygo Goes. Huyu ni mtu ambaye ameleta vijana wengi kutoka Amerika ya Kusini, lakini si wote walifanikiwa kutamba ama kucheza kwa kiwango cha juu.

Lakini sasa ujio wa Vini, umemfanya aongezeke thamani na kuona sasa ameleta suluhisho la kudumu si kuziba pengo la fulani.

Vini anatakiwa kurekebishwa mambo madogo kama alivyowahi kushauri kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Tite. Nakubaliana na Tite kuwa Vini anatakiwa kuboresha kwenye maamuzi yake anapokuwa eneo la hatari na kuongeza uwezo wa kupiga mashuti langoni mwa adui.

Tumeona kwenye mechi kati ya Leganaes akitoa pande murua kwa Luca Vazquez ili apachike bao la pili kwetu. Kisha mwenyewe Vini dakika chache baadaye alipachika bao maridadi kabisa.

Ukirudia kutazama video ya pande la Vini kwenda kwa Lucas Vazquez, lilionyesha ubora wa kufanya maamuzi akiwa lango la adui. Ni kitu muhimu sana. Ameonyesha kuanza kupevuka.Tukigeukia katika akademi ya Castilla imetuletea vijana mahiri kabisa kama Javi Sanchez, Fildrago, Fran Garcia, Franchu, Cristo, Sergio Reguilon, Federico Valverde, Oscar Rodriguez, Achraf Hakimi na Martin Odegaard kwa kuwataja wachache.

Badala ya kuziba viraka, timu inasajili kizazi kipya (inanunua suruali mpya imara zaidi ambayo itakaa mwilini kwa muda mrefu). Inasajili kikosi kipya kama suluhisho la kudumu kwa kizazi cha wachezaji kilichopo ambacho kilisukwa mwaka 2009 na baadaye kuanzia mwaka 2014 hadi 2018 kikaishangaza dunia kwa kutwaa mataji mbalimbali.

Usajili unaofanyika unatafsiri kuwa viongozi wanajenga timu ya kama suluhisho la muda mrefu si kutafuta kisingizio ‘ooh asajiliwe fulani kuziba pengo la fulani’. Timu ambayo anaona kabisa inakuja kutwaa tuzo mbalimbali za dunia.

Watazame Brahim Diaz (19),Vinicius Junior(18), Mohamed Mizzian (17), Chechu (17), Alvaro Odriozola (23), Theo Hernandez (23), Rodrygo Goes (18), Andry Lunin (19).

Wachezaji vijana hadi sasa wanaopewa nafasi kucheza ni Vinicius, Reguilon, Brahim, Federico Valverde, Fildrago, Fran Garcia, Javi Sanchez na wengineo.

Hadi dakika ya mwisho yule beki alibakiza sekunde chache kujiunga na Real Madrid kutoka Espanyol, Hermoso hajasajiliwa. Sababu ni rahisi tu, timu inajivunia kijana wake Javi Sanchez kutoka Castilla akiwa amecheza mechi ya Ligi ya Mabingwa, ligi Kuu na Copa Del Rey kumwongezea uzoefu.

Timu inajieleza kwa vitendo kuwa mabadiliko yanakuja na timu inaelekezwa kwenye kizazi kingine. Tafsiri niliyoona ni kwamba umri wa wachezaji wetu unaruhusu kuwauza, ikiwa na maana anachomolewa mmoja mmoja.

Ukweli mchungu ni kwamba, Zinedine Zidane aliyaona hayo yote. Zidane alitambua kitakachotokea, ndio maana akasisitiza kuwa timu inahitaji mabadiliko na sauti mpya. Nakubaliana naye huyu gwiji.

Naam, kwa hiyo kaondoka Ronaldo na wengine watafuata msimu huu ukimalizika. Kwa hiyo kipindi hiki kumnyooshea kidole mmoja si sahihi. Marekebisho yanahitajika, ndio maana Santiago Solari anaunda jeshi lake jipya kwa kuwapa nafasi vijana ambao hawakupata. Marekebisho ni gharama. TIMU ya Coastal Union ya Tanga iliizamisha klabu ya Yanga bao 1-0, katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu), uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Jumamosi Machi 7, 1992.

Bao hilo pekee lililoizamisha Yanga lilifungwa kwa njia ya penalti na mshambuliaji, Victor Mkanwa, katika dakika ya 17 baada ya mshambuliaji hatari wa Coastal Union, Razak Yusuf 'Careca', wakati anaelekea kufunga bao alibanwa na wachezaji wawili wa Yanga, Said Zimbwe na Abubakar Salum.

Baada ya tukio hilo ndipo mwamuzi wa mchezo huo, Mussa Lyaunga, kutoka Rukwa kuamuru ipigwe penalti kuelekea lango la Yanga na mpigaji, Mkanwa hakufanya makosa akatumbukiza mpira huo kimiani.

Pamoja na wachezaji wa Yanga, wapenzi wao baada ya mchezo huo kumalizika kutoka katika Uwanja wa Mkwakwani kwa huzuni na kuinamisha vichwa chini, pia wachezaji wa timu hiyo walikosa fedha kiasi cha shilingi 500,000 walizoahidiwa na mfadhili wao mkuu, Abbas Gulamali, kama wangeshinda mchezo huo.

Mchezo huo ulianza taratibu, huku kila upande ukiusoma mchezo wa mpinzani wake. Lakini walikuwa ni Coastal Union waliofikia mwanzo goli la Yanga katika dakika ya pili na beki Said Zimbwe alilazimika kutoa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Yanga iliyokuwa ikicheza kwa kujiamini mno walifanya shambulio la kwanza katika dakika ya sita, lakini hata hivyo mpira uliokuwa ukielekezwa langoni na Kenneth Mkapa, ulitolewa kona na beki wa Coastal Union, Said Kolongo.

Baada ya mashambulizi ya huku na kule na kuwafanya mabeki kufanya kazi ya ziada, Yanga ilimkosa beki Joseph Lazaro, katika dakika ya 14 ambaye mwaka wa nyuma yake alichezea timu hiyo ya Tanga baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na David Mwakalebela.

Mpira huo ulimfikia Razak Yusuf ambaye alikuwa ameshaingia katika eneo la hatari na kubanwa na wachezaji wawili wa Yanga, Zimbwe na Salum na mwamuzi akaamuru ipigwe penalti iliyotoa bao la ushindi.

Kupatikana kwa bao hilo kuliamsha ari kwa upande wa Yanga ambao walilisakama lango la Coastal, lakini mabeki wa timu hiyo walisimama kidete kuokoa hatari zote.

Hivyo hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika Coastal Union walitoka kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga vifua mbele kwa kuwafunga Yanga bao 1-0.

Baada ya mchezo huo kumalizika mashabiki wa Coastal Union walionekana kuwa na furaha na walianza kupuliza matarumbeta kutokana na ushindi huo.

Kikosi cha Yanga: Stephen Nemes, Joseph Lazaro/David Mwakalebela, Kenneth Mkapa, Godwin Aswile ‘Scania’, Said Zimbwe (marehemu), Method Mogela ‘Fundi’ (marehemu), Abubakar Salum 'Sure Boy'/Justine Mtekere (marehemu), Hamisi Thobias 'Gagarino' (marehmu),Said Mwamba 'Kizota' (marehemu), Issa Athumani (marehemu) na John Alex.

Kikosi cha Coastal Union: Riffat Said (marehemu), Said Kolongo, Nurdin Kasabalala, Ruben Mgaza, Idrissa Ngulungu (marehemu), Raphael John, Mnjenje Juma, Salum Mohamed, Victor Mkanwa (marehemu),Gordes Mjungu na Razak Yusuf 'Careca'.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.