Kongamano la mwanamke na ajira lafanyika Dar

Mtanzania - - HABARI - Na TUNU NASSOR

SERIKALI imeshauriwa kupunguza vikwazo vya kisheria katika upatikanaji wa alama ya utambulisho (Barcode), ili kuwarahisishia wajasiriamali wanaochipukia katika kukuza biashara zao.

Hayo yamesemwa jana Dar es Salaam na Rais wa Sauti ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania, Maida Waziri, katika kongamano la thamani ya mwanamke na ajira binafsi, lililoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Purple Planet.

Alisema upatikanaji wa barcodes imekuwa na mlolongo mrefu jambo linalowafanya baadhi ya wajasiriamali kushindwa kufuatilia.

“Upatikanaji wa barcodes umekuwa na changamoto nyingi, hasa mlolongo mrefu, hivyo niiombe Serikali ipunguze vikwazo vya kisheria ili wajasiriamali, hasa wadogo, waweze kuipata,” alisema Maida.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili wajasiriamali, hasa wanawake, ni upatikanaji wa vifungashio vya bidhaa wanazozalisha.

“India wana vifungashio vizuri, hivyo tunajaribu kuwasiliana na kampuni za huko ili tupate vifungashio bora,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Purple Planet, Hilda Kisoka, alisema wameandaa kongamano hilo ili kutoa fursa kwa wanawake walio katika sekta isiyo rasmi, kusherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Alisema lengo ni kuwakutanisha wanawake wajasiriamali kujadili fursa na changamoto zilizopo katika shughuli zao za kila siku.

“Kuelekea Tanzania ya viwanda, tumeona ni vema kuwakutanisha wanawake waliojiajiri bila kujali nyanja na matabaka tofauti katika kusherekea Siku ya Wafanyakazi Duniani,” alisema Hilda.

India wana vifungashio vizuri, hivyo tunajaribu kuwasiliana na kampuni za huko ili tupate vifungashio bora. – Maida Waziri

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.