Tenga muda wa familia, kazi

Mtanzania - - Kisima Cha Ujuzi - Na MARKUS MPANGALA

FUNGATE ni kitabu cha nne kutoka kwa mwandishi Fadhy Mtanga. Kitabu hiki kimechapishwa mwaka huu na kampuni ya Gama Printers yenye makao yake wilayani Bagamoyo. Kimepewa nambari ya sikwensia ya ISBN 978-9987-9508-4-3. Mwandishi huyu amewahi kuandika vitabu vingine viwili; Kizungumkuti na Huba.

Fani na Maudhui; Kwa hakika katika kitabu hiki kumekuwa na mambo tofauti na vingine viwili vilivyotangulia. Nimeyashuhudia mabadiliko makubwa mno katika uandishi wa Fadhy Mtanga. Riwaya hii imemleta Fadhy Mtanga mpya kabisa. Misamiati mipya na ufundi.

Maudhui: Msingi wa masimulizi ya riwaya hii ni unaohusisha miji ya Dar es Salaam na Chunya mkoani Mbeya kuhusiana na tukio la Fungate kati ya vijana wawili, Justine Kapufi na Noella Gama, likiwahusisha Antony Mtewa ‘Tony’, Gloria na wazazi wa pande zote mbili.

Tony aliwahi kuwa mpenzi wa Noella kabla ya kutoweka kwa miaka minne. Tony aliondoka Tanzania na kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha. Lakini maisha magumu aliyoyakuta huko Kwazulu Natal akashindwa hata kumiliki simu. Akapoteza mawasiliano.

Baadaye kuliibuka taarifa kuwa alifariki dunia kwenye mapigano kati ya wenyeji na wageni. Ukawa mwisho wa penzi la Tony na Noella.

Kutokana na taarifa za kifo miaka minne baadaye Noella alifunga ndoa na Justine. Baada ya harusi yao wakaelekea kwenye fungate walilofanya jijini Dar es Salaam.

Mwandishi anatuonyesha kila hatua tangu kuanza kwa fungate baada ya kufungwa harusi. Mwandishi anasimulia namna Justine na Noella walivyoianza fungate kabla haijatumbukia kwenye matatizo baina ya mume Justine na mkewe Noella.

Wakati fungate likitarajiwa kuanza, Justine alikuwa na ratiba ya kukutana na mshirika wake wa kibiashara katika hoteli ya Kilimanjaro. Anasema hakukuwa na maelewano ya dhati baina ya Noella na Justine kuwa na ratiba nyingine nje ya fungate.

Pia anatuonyesha mshangao wa Noella badala ya kufurahia fungate na mumewe anajikuta akilazimika kusubiri mpaka amalize kikao cha kibiashara.

Asubuhi wakiwa wanapata kifungua kinywa, Justine na Noella waliketi kwenye mgahawa ambao Tony mpenzi wa zamani wa Noella alikuwapo. Tony aliyerudi nchini kimya kimya, alikuta habari za Noella kuchumbiwa na mwanamume mwingine yaani Justine. Kutokana na heshima yake hakuchukua muda wa kumtafuta, aliacha uhuru wao udumishwe.

Bila kutambua, Noella alikuwa mbele ya Tony aliyeketi nyuma ya viti vya mgahawa huo. Hapo ndipo mwandishi anatuambia Noella aligundua baadaye kuwa Tony yuko hai. Hata alipomaliza kifungua kinywa na kuondoka ilibidi amdanganye mumewe kusahau kitu ili arudi mgahawani kuonana na Tony. Ndivyo ilivyokuwa.

Baada ya mumewe kwenda kwenye kikao cha kibiashara Noella aliondoka kwenda chumba cha hoteli alimofikia Tony, akalala huko hadi alipofumaniwa baada ya kutafutwa kwa muda wa saa 6.

Dhamira kuu inayopatikana katika simulizi hizi ni nafasi ya mwanamke katika kuamua hatima ya maisha yake. Jambo hili tunalipata hapa:

“Ninaomba unisamehe baba. Ninakuomba unipe nafasi ya kuamua ninavyoona inafaa maishani mwangu,”(uk.138). mwandishi anaonyesha namna watoto wa kike au tusema watoto wanavyonyimwa nafasi ya kuamua hatima ya maisha yao. Licha ya matatizo yaliyomkuta mhusika mkuu Noella, mwandishi anamtumia kufikisha ujumbe kwa jamii.

Aidha, mwandishi anaonyesha makosa ya Justine ambaye huwakilisha tabaka na watu wanaochapa kazi bila kupumzika au kutopata muda wa kuwa familia. Mwandishi anamtumia Noella kwa mara nyingine kutafakari kwa upana maana ya fungate.

“Fungate ni utamaduni kwa wanandoa wapya. Ni utamaduni wa wao kwenda mahali pa peke yao wasikokutana na watu waliowazoewe kwenye maisha yao ya kawaida. Hii ni nafasi ya kudumisha ukaribu na uhusiano wao wa ndoa. Nafasi adhimu kwa wanandoa hao kufurahia ndoa yao pasipo kubughudhiwa na pilika za kila siku za maisha yao. Fungate hufaa zaidi endapo wanandoa hao watakwenda mahali mbali na maeneo yao ya mazoea. Huko watakutana na hali ya kimahaba ambayo huwafanya wafurahie zaidi. Huwafanya upendo baina yao kuota mizizi huku ukifungua mwanzo mzuri wa ndoa yao,” Noella alitafakari (uk40-41).

Nafasi ya familia; mwandishi ameonyesha umuhimu mkubwa wa familia. Anasema ni vizuri kutenga muda wa familia na kazi. Masimulizi ya mwandishi huyu yamenikumbusha Profesa mmoja aliyejilaumu kwa kutotoa kipaumbele kwa familia yake na kujikita kupata sifa za kisomi. Aligundua baadaye makosa yake.

“Maisha haya, usiwaone watu wanatembea barabarani wakipendeza. Kuna watu wana siri nyingi za misoto waliyowahi kupitia ili kuwa vile walivyo. Maisha ni kama tanuri la moto,” Tony alisema (uk.67).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.