Wazama baharini kuokota taka za plastiki

Mtanzania - - HABARI - Na VERONICA ROMWALD -DAR ES SALAAM

WAZAMIAJI zaidi ya watano wamezama ndani ya Bahari ya Hindi na kwenda kukusanya taka mbalimbali zilizozama, hasa za plastiki kisha kuzitoa nje ya bahari.

Tukio hilo limefanyik­a Dar es Salaam jana katika Ufukwe wa Yacht Club, ikiwa ni kilele cha maadhimish­o ya Wiki ya Mazingira Duniani, ambayo kwa mwaka huu yalipewa kaulimbiu ya pambana dhidi ya matumizi ya bidhaa za plastiki.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Vedast Makota, alisema tatizo la uchafuzi wa mazingira hasa katika fukwe, ni kubwa nchini.

Alisema ili kukabili changamoto hiyo, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa jamii kuhusu athari za mifuko ya plastiki, hasa inapofika na kuzama baharini.

“Utaona mwaka 2006 kuna mkakati wa haraka ambao ulitolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais wa kudhibiti uchafuzi wa fukwe, ikiwamo za bahari, maziwa na mito,” alisema.

Pia alisema mkakati huo unatoa maelekezo kwa halmashaur­i zote nchini kuhakikish­a zinaweka mipango madhubuti ya kuhakikish­a wanakabili­ana na changamoto hiyo.

“Pia mwaka huo huo Serikali ilitoa kanuni ya kudhibiti utengeneza­ji, ununuzi na matumizi ya mifuko yenye kiwango cha chini ya microns chini ya 30,” alisema.

Alisema mwaka 2005 Serikali ilitengene­za tena mkakati mwingine kwa kuongeza kiwango cha hadi kufikia microns isiyozidi 50.

“Lengo letu ni kupunguza matumizi ya mifuko ya plastiki, hasa ile midogo midogo ambayo ilikuwa kero kubwa,” alisema.

Pia alisema ni vema wananchi wakajenga utamaduni wa kukusanya taka, hasa za mifuko ya plastiki ili isiishie baharini na hivyo kuathiri uhai wa viumbe hai baharini.

“Tukio la leo (la kuzama) baharini limetoa mwanga na itakuwa vema wenzetu wenye uwezo wa kuzama ili kutoa taka hizi, itakuwa vizuri wakitusaid­ia kwa sababu zikibaki kule chini ni hatari kwa viumbe hai,” alisema.

Naye, Foster Mkapa ambaye ni mwanachama wa Lions Club ya Dar es Salaam (Tanzanite), alisema juhudi zinahitaji­ka kupambana na hali hiyo.

“Ikiwa hatutafany­a jitihada za kudhibiti mifuko ya plastiki, maana yake ni kwamba vizazi vijavyo havitakuja kupata vitoweo vya baharini, hasa samaki,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.